Hamas yasema itawaachia mateka zaidi wa Israel
14 Februari 2025Kundi la Hamas limesema litaendelea na mipango ya kuwaachia huru mateka watatu zaidi wa Israel, hatua inayotarajiwa kumaliza mvutano mkubwa uliouweka rehani mkataba wa kusitisha vita kwenye Ukanda wa Gaza.
Hamas inayotawala eneo hilo la Wapalestina ilitishia mapema wiki hii kuchelewesha awamu ijayo ya kuwaachia huru mateka wa Israel ikiituhumu nchi hiyo kukiuka vipengele vya makubaliano ya kusitisha vita kwa muda wa siku 42.
Soma pia:Machozi na shangwe kwa Wapalestina walioachiwa Ukingo wa Magharibi
Israel iliyopata uungwaji mkono wa Marekani ilisema ingeanzisha upya vita kwenye Ukanda wa Gaza iwapo Hamas haitowaachia huru mateka wake ifikapo Jumamosi.
Hamas imesema imefanya mazungumzo na maafisa wa Misri mjini Cairo na inawasiliana na Waziri Mkuu wa Qatar juu ya kutumwa msaada zaidi wa mahema, vifaa vya matibabu, mafuta na matingatinga ya kufanya ukarabati kwenye Ukanda wa Gaza.
Hapo kabla Hamas iliilaumu Israel kuzuia uingizwaji wa kutosha wa mahitaji hayo ambayo ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha vita.