Hamas yasema itawaachia mateka sita wa Israel
18 Februari 2025Kundi la Hamaslimetangaza kuwa litawaachia mateka sita wa Israel Jumamosi ijayo, na miili ya mateka wengine wanne Alhamisi wiki hii. Ofisi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, imethibitisha kwamba makubaliano hayo yamefikiwa na Hamas mjini Cairo leo.
Ni pamoja na miili ya wanafamilia ya Bibas, ambao kwa Waisraeli wengi wamekuwa kama sura ya masaibu wanayopitia mateka huko Gaza. Israel imesema ina wasiwasi mkubwa kuhusu Bi Shiri Bibas na watoto wake wawili wadogo wa kiume, Ariel na Kfir, lakini haijathibitisha vifo vyao. Hamas inasema waliuawa katika shambulizi la angani la Israel mwanzoni mwa vita.Israel kujadili awamu inayofuata ya amani kwa Gaza
Kiongozi wa Hamas Khalil al-Hayya, katika taarifa iliyorekodiwa amesema leo kuwa familia ya Bibas itajumuishwa kwenye mpango wa kukabidhi miili minne. Ni miili ya kwanza kukabidhiwa kwa Israel chini ya makubaliano ya sasa ya kusitisha mapigano. Wakati huo huo, wizara ya mambo ya nje ya Misri imesema kuwa mkutano wa kilele utakaojadili mpango uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump wa kuwahamisha wakazi wa Gaza, utafanyika mjini Cairo Machi 4 ili kuwezesha maandalizi zaidi ya mipangilio thabiti.