Hamas yasema iko tayari kwa makubaliano
4 Septemba 2025Hamas imesema bado inasubiri majibu kutoka Tel Aviv juu ya pendekezo la hivi punde zaidi lililowasilishwa na wapatanishi wa kimataifa.
Israel imeendelea kusisitiza masharti yake kuwa makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano yanapaswa kuambatana na kuachiliwa kwa mateka wote walioko mikononi mwa Hamas pamoja na kundi hilo kusalimisha silaha. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amepuuza maneno ya Hamas akisema, "Hamas inaendelea kudanganya na kutoa maneno matupu.”
Taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, imeyataja matamshi ya Hamas kama hadaa tu na hayana jipya.
Hamas, kwa upande wake, imesema iko tayari kufanya makubaliano ya kubadilishana wafungwa, ikiwemo kuwaachia huru mateka wote wa Israel walio mikononi mwao kwa masharti ya kuachiwa idadi itakayokubaliwa ya wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel. Kundi hilo pia limeeleza utayari wake wa kuundwa kwa serikali huru ya wataalamu watakaousimamia Ukanda wa Gaza, lakini Hamas hawakujibu kuhusiana na masharti mengine ya Israel kwa ajili ya kusitisha vita.
Huko Jerusalem, mamia ya Waisraeli wameandamana kutaka yafikiwe makubaliano ya kusitisha vita na kuachiwa kwa mateka walioko Gaza, karibu miaka miwili tangu vita vilipoanza.
"Tumekuja hapa kupaza sauti kwa mateka ambao tunataka kuwaona wakirudi nyumbani. Tunaona picha zinazotoka kwa Hamas. Wanaonekana katika hali mbaya sana. Hali yao, hasa kiafya, si nzuri. Ni kama siku za mwisho ambazo tunaweza kufanya sauti yao isikike, ili tuwaone wakirudi nyumbani kwa familia zao. Tunatumaini kwa dhati kwamba serikali itatusikiliza na kuchukua uamuzi wa kuwaokoa." Alisema mmoja wa waandamanaji.
Waasi wa Kihouthi wazidisha mashambulizi
Katika hatua nyingine Waziri wa Ulinzi wa Israel, ameapa kuwaadhibu vikali waasi wa Kihouthi wa Yemen ambao wamezidisha mashambulizi yao ya makombora dhidi ya Israel.
Kauli hii imetolewa baada ya kombora jingine kurushwa kutoka Yemen kuelekea Israel mapema Alhamisi, ikiwa ni shambulio la tatu ndani ya saa 24. Jeshi la Israel limesema kombora hilo lilianguka katika eneo wazi nje ya mipaka ya Israel na halikusababisha madhara yoyote.
Huku haya yakijiri, hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota katika Ukanda wa Gaza. Maafisa wa kijeshi wa Israel wametangaza kuwa mashambulizi yao ya hivi karibuni kwenye Jiji la Gaza huenda yakasababisha wakazi wapatao milioni moja kulazimika kuhama makazi yao. Taarifa hiyo imetolewa huku mashirika ya misaada yakionya kuhusu njaa kali na hali mbaya ya usalama kwa raia.