Hamas yapinga wazo la Trump la kuwahamisha Wapalestina Gaza
10 Februari 2025Akirejea Jumapili usiku kutoka Marekani alikokuwa ziarani, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliisifu kauli ya rais wa Marakani Donald Trump ya kutaka kuchukua udhibiti wa Gaza na kuwahamisha Wapalestina kwenye mataifa ya Misri na Jordan akisema kuwa ni "hatua ya kimapinduzi".
Siku ya Jumapili, Trump alizidi kuuchochea moto kuwa yuko tayari kujitolea kuinunua na kuimiliki Gaza, lakini anaweza kuruhusu sehemu ya ardhi iliyoharibiwa na vita kujengwa upya na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati ambayo hata hivyo hakuyataja.
Kiongozi wa Hamas Khalil al-Hayya amepinga wazo hilo na kusema watapambana kikamilifu hadi mpango huo ushindwe kama ilivyoshindwa mipango mingine hapo kabla. Al-Hayya aliyasema hayo jana mjini Tehran wakati wa maadhimisho ya miaka 46 ya mapinduzi ya serikali ya Kiislamu ya Iran.
Wazo la Trump liliibua ukosoaji mkubwa kote ulimwenguni hasa kwa mataifa ya kiarabu na kiislamu. Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wakiwa viongozi wa hivi karibuni kuupinga mpango huo. Kabla ya kuabiri ndege kuelekea Malaysia, Erdogan alisema:
"Hakuna mwenye uwezo wa kuwahamisha Wapalestina kwenye ardhi yao ya milele ambayo wamekuwepo kwa maelfu ya miaka. Palestina, ikiwa ni pamoja na Gaza, Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ni mali ya Wapalestina. Watu wa Gaza, ambao hawakuondoka katika ardhi yao licha ya ukatili na mashambulizi yote ya Israel, wataendelea kubaki, kuilinda na kuishi Gaza."
Israel yaanza kuwaondoa wanajeshi wake Gaza
Afisa kutoka wizara ya mambo ya ndani inayoongozwa na Hamas huko Gaza amesema majeshi ya Israel yameondoa vifaru na vizuizi vyao katika ujia wa Netzarim kwenye Barabara ya Salaheddin, na hivyo kuruhusu magari kupita kwa uhuru kuelekea kaskazini mwa ukanda wa Gaza.
Licha ya Israel na Hamas kubadilishana mateka na wafungwa kama sehemu ya makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza, bado kuna wasiwasi iwapo awamu ya pili ya mpango huo itatekelezwa ipasavyo kutokana na pande zote katika mzozo huo kutoonyesha nia thabiti ya kushiriki kikamilifu katika mazungumzo yaliyotarajiwa kuanza Februari 3 mjini Doha, huko Qatar.
(Vyanzo: Mashirika)