Hamas yaliangalia upya pendekezo la kusitisha vita Gaza
4 Julai 2025Tangazo hilo linakuja kabla ya ziara ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Washington, ambako Rais Trump anapigia debe mpango wa kumaliza vita. Mapigano hayo yalianza Oktoba 7, 2023, kufuatia shambulio la Hamas dhidi ya Israel, na kusababisha mashambulizi makali ya Israel kwa lengo la kuiangamiza Hamas na kuwaokoa mateka.
Mapatano ya awali ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Qatar, Misri na Marekani yalisababisha kuachiliwa kwa baadhi ya mateka wa Israel kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina. Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa asubuhi, Rais Trump alisema "tutaona kinachotokea. Tutajua ndani ya saa 24 zijazo."
Mashambulizi ya Israel yamewauwa zaidi ya Wapalestina 90 Gaza
Vyanzo vya mazungumzo vinaeleza kuwa pendekezo hilo linahusisha usitishaji wa mapigano kwa siku 60, ambapo Hamas itaachilia nusu ya mateka walioko hai, na Israel nayo itawaachia baadhi ya wafungwa wa Kipalestina.
Wakati pande zote zikisubiri suluhu, hali ya kibinadamu Gaza inazidi kuwa mbaya. Kulingana na taarifa mpya, Wapalestina 300 wameuawa ndani ya masaa 48 yaliyopita kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel, wengi wao wakiwa katika harakati za kutafuta msaada wa chakula karibu na vituo vya usambazaji wa misaada.
Amnesty yaukosoa mfumo wa misaada unaoungwa mkono na Israel na Marekani
Amnesty International imekosoa mfumo huo wa misaada unaoungwa mkono na Israel na Marekani, ikisema ni mbinu ya kutumia njaa kama silaha ya vita. Shirika hilo limesema: “Israel imegeuza hali ya kusaka misaada kuwa mtego wa kuwanasa Wapalestina wanaokufa njaa kupitia vituo vinavyodhibitiwa kijeshi vya GHF.”
Takwimu kutoka Wizara ya Afya ya Gaza zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 500 wameuawa katika au karibu na vituo hivyo ndani ya mwezi mmoja uliopita, huku baadhi ya walinzi binafsi wakikiri kuwafyatulia risasi raia wanaotafuta msaada.
Amnesty International: GHF yatumika kuwauwa Wapalestina
Mashirika zaidi ya 160 ya kimataifa yametoa wito wa kusitishwa kwa mfumo huo wa usambazaji misaada, yakisema unakiuka misingi ya kibinadamu. Hata hivyo, Israel imekanusha shutuma hizo na kuvituhumu vyombo vya haki za binadamu kuwa vinashirikiana na Hamas kwa ajili ya propaganda.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya 57,000 wameuawa Gaza tangu Oktoba 2023, wengi wakiwa raia, huku mashambulizi ya Oktoba 7 yakiua watu 1,219 nchini Israel. Pamoja na machungu hayo, shinikizo la kimataifa linaongezeka kwa pande zote kukubaliana na kusitisha mapigano.