Hamas yakubali pendekezo jipya la kusitisha mapigano
18 Agosti 2025Afisa mwandamizi wa kundi la Hamas Bassem Naim ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba wanamgambo hao wamekubaliana na pendekezo hilo liliandaliwa na wapatanishi, ingawa hakutoa maelezo zaidi.
Afisa mmoja wa Misri, akizungumza na AP kwa sharti la kutotambulishwa kwa kuwa haruhusiwi kuzungumzia suala hilo, amesema pendekezo hilo linajumuisha mabadiliko juu ya sharti la Israel kuwaondoa wanajeshi wake kwenye Ukanda wa Gaza pamoja na dhamana ya mazungumzo juu ya usitishaji wa kudumu wa mapigano kama walivyokubaliana awali.
Afisa huyo amesema pendekezo hili la sasa linakaribia kufanana na pendekezo la awali lililoidhinishwa na Israel, ambayo bado haijajiunga kwenye mazungumzo haya ya karibuni. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameapa kuviendeleza vita hivyo hadi mateka wote watakapoachiliwa na Hamas, kundi hilo kupokonywa silaha pamoja na usalama wa kudumu wa Gaza.
Lakini Hamas imesema itawaachilia tu mateka waliosalia ikiwa itahakikishiwa usitishwaji wa kudumu wa mapigano na Israel kuondoka kwenye eneo hilo.
'Juhudi za kina' kufufua mazungumzo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty alisema wapatanishi "wanajaribu kwa kila hali" kulifufua pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano kwa siku 60, wakati ambapo baadhi ya mateka wataachiliwa na pande zote kuwa na nafasi ya kujadili usitishaji vita wa kudumu na kuwarudisha mateka wengine.
Amesema hayo alipokitembelea kivuko cha Rafah kinachounganisha Misri na Gaza, ambacho haijafanya kazi tangu Israel ilipolidhibiti eneo hilo la Palestina Mei 2024. Aliandamana na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina Mohammad Mustafa, ambaye kwa kiasi kikubwa amewekwa pembeni tangu vita hivyo vilipoanza, Oktoba, 2023.
Abdelatty amesema Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani alijiunga kwenye mazungumzo hayo pamoja na kiongozi mkuu wa Hamas Khalil al-Hayya, aliyewasili Cairo wiki iliyopita.
Alisema wapo wazi kwa mapendekezo mengine, ikiwa ni pamoja na mpango wa kina ambao ungepelekea mateka wote kuachiliwa mara moja.