Hamas yakubali pendekezo la Misri la kusitisha mapigano
19 Agosti 2025Afisa mmoja wa Israel amethibitisha kuwa nchi hiyo imepokea majibu ya Hamas ingawa hadi sasa hakuna jibu rasmi lililotolewa na Tel Aviv kuhusu mpango huo wa hivi karibuni wa kusitisha mapigano.
Mpango huo wa kusitisha mapigano umetolewa baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya awali ya mwezi Machi, ambayo pia yalihusisha ubadilishanaji wa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina wanaozuiliwa katika magereza ya Israel. Mashambulizi yanayofanywa na Israel yameiharibu vibaya Gaza, na kuwasukuma wakaazi wengi katika ukanda huo wakikodolea macho njaa ya kutisha.
Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imeripoti vifo vya zaidi ya watu 62,000 tangu Oktoba mwaka 2023, huku takriban watu 263 wakiwemo watoto 112 tayari wamefariki kutokana na njaa.
Katika ngazi ya kidiplomasia, Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani walikutana mjini Cairo jana Jumatatu kuhusu kadhia ya Gaza.
Viongozi hao wawili walitoa mwito wa usitishaji mapigano mara moja na pia wamepinga vikali jaribio lolote la kuikalia tena Gaza au kuwafurusha Wapalestina kutoka ardhi yao. Wamesisitiza kwamba kuundwa kwa taifa huru la Palestina ndio njia pekee ya kudumu kuelekea kupatikana amani na uthabiti wa muda mrefu katika mzozo huo.
Waandamanaji washinikiza makubaliano ya kumaliza vita
Shinikizo la kufikia makubaliano limekuwa likiongezeka hata ndani ya Israel. Mnamo siku ya Jumanne, waandamanaji walifunga barabara kuu mjini Tel Aviv wakishinikiza kufikiwa kwa mkataba wa kuwarudisha nyumbani mateka waliobaki na kuvimaliza vita hivyo.
Makumi kwa maelfu ya watu waliwahi pia kuandamana tangu vita hivyo vilipoanza wakionya kuwa mipango ya serikali ya Tel Aviv ya kuutwaa ukanda wa Gaza itazidisha zaidi mgogoro huo.
Shai Moses, ni raia wa Israel aliyeshiriki maandamano hayo. "Tulianza Jumapili kuishinikiza Israel ili kuwarudisha mateka wetu, tumegundua kwamba njia pekee inayofanya kazi ni kuiwekea shinikizo serikali kufikia makubaliano, kuyakamilisha na kuwarusisha mateka nyumbani na kusitisha vita. Hatutaacha kufanya hivyo hadi mateka wote warudi nyumbani."
Wakati hayo yanaendelea, huko mjini Washington, kumeibuka utata baada ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani kutangaza kwamba inasitisha utoaji wa viza za wageni kwa Wapalestina kutoka Gaza.
Uamuzi huo umefuatia madai yaliyotolewa na mwanaharakati anayeegeemea siasa za mrengo mkali wa kulia Laura Loomer kwamba wakimbizi walikuwa wanaingia Marekani kwa kutumia mpango huo wa viza za wageni.
Marekani yasitisha utoaji wa viza kwa Wapalestina wa Gaza
Wakosoaji wa uamuzi huo, likiwemo baraza la mahusiano ya Kiislamu nchini Marekani na shirika la misaada la HEAL Palestine, wametahadharisha kwamba usitishaji huo wa viza kutawaathiri watoto waliojeruhiwa vibaya na ambao wanahitaji matibabu nje ya nchi.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeeleza kwamba imetoa maelfu ya viza kwa ajili ya matibabu kwa Wapalestina mwaka huu, japo maafisa wamekiri kuwa idadi ndogo ya viza imetolewa kwa Wapalestina katika ukanda wa Gaza hivi katika siku za hivi karibuni.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesisitiza kwamba viza hizo hazihusiani kabisa na mpango wa kuwapa makaazi wakimbizi bali ni kwa ajili ya matibabu ya muda tu. Uamuzi wa wizara hiyo ya mambo ya nje ya Marekani wa kusitisha utoaji wa viza umekoselewa na mashirika ya haki na binadamu yalioishtumu Washington kwa kusalimu amri kufuatia shinikizo la kisiasa.
Kwengineko, mvutano wa kidiplomasia umejitokeza kati ya Israel na Australia. Hii ni baada ya Israel kufuta viza za wanadiplomasia wa Australia walioko katika Mamlaka ya Palestina baada ya Australia kulitambua taifa la Palestina huku nchi hiyo ikienda mbali zaidi na kufuta viza ya mbunge wa Israel aliyekuwa akipigia debe kunyakuliwa kwa eneo la Ukingo wa Magharibi.
Waziri wa mambo ya nje wa Australia Penny Wong ameitaja hatua ya Israel kuwa "isiyo na msingi” na ameishtumu serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa kujitenga na dunia katika wakati ambapo diplomasia inahitajika zaidi.