Hamas yakubali kuwaachia mateka kumi wa Israel
10 Julai 2025Taarifa ya Hamas ilitolewa baada ya siku nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yaliyosimamiwa na Qatar, huku Marekani ikionyesha imani kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku 60 yatafikiwa kabla ya mwisho wa juma hili.
Aidha Israel ikiongeza kwamba bado kuna vikwazo katika mazungumzo hayo ikiwemo suala la kuingia kwa misaada ndani ya Gaza, kuondoka kwa vikosi vya Israel katika eneo hilo na kile walichokiita 'dhamana halisi ya amani ya kudumu'.
"Licha ya ugumu wa mazungumzo juu ya masuala haya hadi sasa kutokana na ukaidi wa Israel, tunaendelea kushirikiana kwa dhati na kwa moyo na wapatanishi ili kushinda vikwazo hivyo, kumaliza mateso ya watu wetu, na kuhakikisha wanatimiza matarajio yao ya uhuru, usalama, na maisha yenye heshima,” sehemu ya taarifa ya Hamas ilisema.
Mapema, Israel ilionekana kuunga mkono matumaini ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu kumalizika kwa vita hivyo, wakati mazungumzo mjini Doha yakiingia siku ya nne huku kukiwa na taarifa ya kutoridhika kuhusu msimamo wa Israel juu ya misaada ya kibinadamu.
Mkuu wa majeshi ya Israel, Eyal Zamir, amesema katika hotuba ya televisheni kuwa hatua za kijeshi zilizochukuliwa hadi sasa zimeandaa mazingira ya kufikiwa kwa makubaliano ambayo yenye matokeo ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel nyumbani.
Awali, afisa mwandamizi wa Israel akiwa katikati mwa ziara ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu huko Washington alisema, iwapo pande zote mbili zitakubaliana na pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku 60, Israel itatumia muda huo kutoa pendekezo la kusitisha mapigano kabisa na Hamas kutakiwa kupokonywa silaha.
"Ikiwa Hamas itakataa, tutaendelea na operesheni za kijeshi huko Gaza." Alisema afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Rais Donald Trump wa Marekani alikutana kwa mara ya pili na Waziri Mkuu Netanyahu kujadili hali ya Gaza, huku mjumbe wa rais wa Marekani Mashariki ya Kati akionyesha kuwa Israel na Hamas walikuwa karibu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopendekezwa na Marekani baada ya vita vya miezi 21.
Hapo awali Trump alitabiri huenda makubaliano yangelifikiwa ndani ya juma hili, hali iliyozua tetesi kuhusu uwezekano wa kutangazwa kabla ya Netanyahu kurejea Israel siku ya Alhamisi.
Mjumbe maalum wa Trump Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumanne kuwa makubaliano yaliyotarajiwa yangelikuwa na kipengele cha kuachiliwa kwa mateka 10 walio hai na 9 waliokufa.
Israel yaendeleza mashambulizi ndani ya Gaza
Shirika la ulinzi wa raia la Gaza limesema kuwa watu 23, wakiwemo watoto wanane, wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel usiku ya kuamkia leo.
Afisa wa shirika hilo, Mohammed al-Mughair, alisema wimbi la hivi karibuni la mashambulizi lililenga maeneo ya kati na kusini mwa Gaza, ambapo shambulio baya zaidi liliua watu 12 katika mji wa Deir el-Balah.
Watoto wanane na wanawake wawili ni miongoni mwa waliouawa, na kuongeza kuwa ndege za kijeshi za Israel zililenga "mkusanyiko wa raia mbele ya kituo cha matibabu.”
Jeshi la Israel halijatoa tamko lolote kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni ya Gaza.
Wahouthi watumia muda huu kuishambulia Israel
Jeshi la Israel limesema limedungua kombora lililovurumishwa na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran na kufuatiwa na mkururo wa mashambulizi ya Israel katika maeneo ya Wahouthi.
Kupitia mtandao wa X Israel imesema kombora hilo lilidunguliwa na kuharibiwa baada ya ving'ora vya tahadhari kulia mapema leo alfajiri kwenye maeneo kadhaa nchini humo.
Msemaji wa kijeshi wa Houthi Yahya Saree amekiri Houthi kuhusika na mashambulizi hayo ya kuunga mkono watu wa Palestina na kusema kwamba yalikuwa yenye mafanikio makubwa.
"Jeshi la wanamgambo wanathibitisha kuwa wataendelea kupanua oparesheni zake kwa mashambulizi ya makombora dhidi ya malengo ya kijeshi ya kimkakati huko Palestina inayokaliwa kimabavu."