Hamas yakridhia pendekezo la usitishwaji mapigano Gaza
26 Mei 2025Pendekezo hilo linajumuisha kuachiwa mateka10 wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas pamoja na uwepo wa siku 70 za usitishaji mapigano. Pendekezo hilo pia linazingatia kuachiwa wafungwa wakipalestina wanaoshikiliwa na Israel ikiwemo mamia ya wale wanaotumikia vifungo vya muda mrefu.
Duru hiyo imeliambia shirika la habari la AFP kwamba mazungumzo ya kusitisha kikamilifu mapigano yatafanyika wakati wa utulivu huo wa siku 70.
Haya yanajiri wakati kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, akisema hatua za Israel katika Ukanda wa Gaza haziwezi tena kuhalalishwa hasa mstari mwekundu unapovukwa au sheria ya kimataifa ya kibinaadamu inapokiukwa.
Ujerumani yaikosoa Israel kwa vita vyake huko Gaza
"Lazima niseme kwamba kile kilichotokea wikiendi, kushambuliwa shule nyengine katika ukanda wa Gaza ni janga la kibinadamu. Tuna mawasiliano ya karibu sana na serikali ya Israel. Nitazungumza na Netanyahu wiki hii. Lazima niseme kwa uwazi zaidi kuhusu kile jeshi la Israel linachofanya katika Ukanda wa Gaza. Kusema kweli, sielewi tena kwa nini watu wanaumia kiasi hiki. Hili haliwezi tena kuhalalishwa; haya sio mapambano dhidi ya Hamas Huo ni mtazamo wangu," alisema Kansela huyo wa Ujerumani.
Israel bado haijatoa tamko lolote kuhusu kauli hiyo.