Hamas yachunguza kosa katika kutambua mwili wa Shiri Bibas
21 Februari 2025Hamas ilipaswa kukabidhi miili ya na watoto wake wawili wa kiume, Kfir na Arile siku ya Alhamisi, pamoja na mabaki ya mateka wa nne chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yaliofikiwa mwezi uliopita.
Miili minne ilikabidhiwa ambapo utambulisho watoto wa Biba na mateka wa nne Oded Litshitz ulithibitishwa. Lakini wataalamu wa Israel walisema mwili wa nne ulikuwa wa mwanamke ambaye hakutambuliwa na siyo Bibas, alietekwa pamoja na watoto na mume wake Oktoba 7, 2023.
Basem Naim, mjumbe wa kamati ya kisiasa wa Hamas, amesema kosa hilo la bahati mbaya linaweza kutokea, hasa kwa sababu mashambulizi ya Israel yalichanganya maiti za mateka wa Israel na Wapalestina, ambao maelfu yao bado wamefukiwa kwenye vifusi.
Netanyahu: Hamas italipa kwa kutorejesha mabaki ya Shiri Bibas
Naim alisema katika taarifa kuwa siyo katika maadili au maslahi yao kuhodhi miili yoyote au kutotekeleza mikataba na makubaliano waliosaini. Katika hatua tofauti, Hamas imesema itachunguza madai ya Israel na kutangaza matokeo.
Kushindwa kukabidhi mwili wa Shiri na makabidhiano ya majeneza yaliyofanywa hadharani siku ya Alhamisi, kumesababisha ghadhabu nchini Israel, na kitisho cha kulipiza kisasi kutoka kwa Netanyahu. Hamas ilisema mwezi Novemba 2023 kwamba watoto hao na mama yao waliuawa katika shambulio la anga la Israel, na mkurugenzi wa ofisi ya habari ya Gaza Ismail al-Thawabta, alisema Netanyahu anawajibika kikamilifu kwa mauaji yao.
Israel yasema mateka waliuwawa kwa maksudi
Lakini jeshi la Israel limesema tathmini ya intelijensia na uchunguzi wa mabaki ya watoto wa Bibas vinaonyesha waliuawa kwa maksudi na watekaji wao.
Netanyahu hakufafanua jibu atakalotoa, lakini tukio hilo linatilia mkazo utepetepe wa makubaliano ya kusitisha vita, yaliofikiwa kwa shinikizo la Marekani na msaada wa wapatanishi wa Qatar na Misri mwezi ulipita.
Ujerumani yasema mataifa mawili huru ndiyo suluhu pekee Mashariki ya Kati
Tawi la Kijeshi la Hamas limesema litawaachia mateka sita wa Israel hapo kesho, na kuwataka kuwa ni Eliya Cohen, Omer Shem Tov, Tal Shoham, Mer Wenkert, Hisham al-Sayed na Avera Mengisto. Hisham al-Sayed na Avera ni raia walioingia Gaza muongo mmoja uliopita na kushikiliwa huko tangu wakati huo. Katika kubadilishana, Israel itawaachilia wafungwa 602 wa Kipalestina kutoka jela zake, wakiwemo 445 kutoka Gaza, waliokamatwa baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7, 60 wanaotumikia vifungo virefu, 50 wanaotumikia vifungo vya maisha, na 47 waliokamatwa tena baada ya mabadilishano ya wafungwa ya mwaka 2011.
Yote hayo yanajiri wakati viongozi wa mataifa ya Kiarabu wanakutana nchini Saudi Arabia kuandaa mpango wa kuijenga upya Gaza, wakinuwia kuziwia mpango wa Rais Donald Trump wa kuliweka eneo hilo chini ya udhibiti wa Marekani na kuwafukuza wakazi wake.
ap,reuters,afp