Hamas tayari kwa mazungumzo mengine ya amani
27 Februari 2025Kundi hilo linalotawala ardhi hiyo ya Wapalestina limeelezea utayari huo baada ya hapo jana kukabidhi miili ya mateka wa wanne wa Israel na kuwapokea wafungwa 600 wa Kipalestina waliokuwa wanazuiliwa kwenye jela nchini Israel.
Mabadilishano hayo ndiyo ya mwisho katika utekelezaji wa awamu ya kwanza mkataba wa kusitisha vita kwa muda wa siku 42 ambazo zinakamilika mwishoni mwa juma hili.
Majadiliano kuhusu awamu ya pili ya usitishaji mapigano ambayo yatahusiha kuachiwa huru kwa mateka zaidi wa Israel bado hayajaanza. Kwenye taarifa yake ya leo kundi la Hamas limesema "njia pekee" kwa Israel kuwapata mateka waliobakia ni kufanya mazungumzo ya kupata mkataba mpya likionya Tel Aviv kwamba hatua yoyote ya kurudi nyuma "itaongeza madhila kwa mateka hao na familia zao"