Israel na Hamas kubadilishana wafungwa na mateka
26 Februari 2025Msemaji wa Hamas, Abdul Latif al-Qanou ameliambia shirika la habari la AP kwamba kundi hilo la wanamgambo litaikabidhi miili ya mateka wanne wa Israel Alhamisi kwa kubadilishana na mamia ya wafungwa wa Kipalestina, siku chache kabla ya kumalizika kwa makubaliano ya kwanza ya kusitisha mapigano Gaza baina ya pande hizo hasimu.
Wafungwa 600 walitakiwa kuachiwa wiki iliyopita
Israel ilichelewesha kuwaachia takribani wafungwa 600 wa Kipalestina, tangu Jumamosi iliyopita, kupinga kile ilichokisema ni unyanyasaji wa kikatili wa mateka wakati wa kuachiliwa kwao na Hamas.
Kwa upande wake Hamas ilisema hatua ya Israel kuchelewesha kuwaachia wafungwa hao wa Kipalestina, ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya kusitisha mapigano, na kwamba duru ya pili ya mazungumzo haitowezekana hadi watakapoachiliwa huru.
Hayo yanajiri wakati ambapo mazishi ya Shiri Bibas na watoto wake wawili wa kiume Ariel na Kfir yakiwa yanafanyika Jumatano. Umati mkubwa wa watu umekusanyika katikati ya Israel kwa ajili ya kuhudhuria mazishi hayo ya familia ya Bibas.
Shiri na watoto wake walitekwa nyara Oktoba 7, 2023 na kupelekwa Gaza. Miili ya watoto hao ilirudishwa Israel Alhamisi iliyopita, huku mwili wa mama yao ukirudishwa Ijumaa, baada ya hapo awali familia yake kukabidhiwa mwili ambao sio wake.
WHO: Asilimia 92 ya watoto Gaza wapata chanjo ya polio
Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani, WHO limesema zaidi ya asilimia 92 ya watoto wenye chini ya umri wa miaka 10 huko Gaza, wamepokea chanjo ya polio katika duru ya pili ya kampeni ya kutoa chanjo hiyo. Dokta Rik Peeperkorn, mwakilishi wa WHO katika Mamlaka ya Palestina inayokaliwa kimabavu, amesema shirika hilo lina wasiwasi kuhusu operesheni zinazoendelea za Israel kwenye kambi za wakimbizi katika Ukingo wa Magharibi, na athari zake katika huduma za afya.
''Kuna takribani watu 40,000 wasio na makaazi. Mashambulizi 44 ya mwaka huu yameathiri utoaji wa huduma ya afya katika Ukingo wa Magharibi. Sisi kama WHO, tunajaribu kusaidia kupeleka vifaa mapema iwezekanavyo, katika hospitali kuu ya Ukingo wa Magharibi. Pia tunatoa huduma ya ushauri nasaha kwa watu wenye kiwewe,'' alifafanua Dokta Peeperkorn.
Peeperkorn amesema tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Israel na Hamas Oktoba 2023, miundombinu ya huduma za afya Gaza imeharibiwa vibaya, na uharibifu unakadiriwa kufikia dola bilioni 6.3 za Kimarekani.
Soma zaidi: Netanyahu asema anaunga mkono mpango wa Trump kuhusu Gaza
Ama kwa upande mwingine, mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Anwar Gargash amesema Jumatano kuwa mpango wa ujenzi mpya wa Gaza hauwezi kufanyika bila ya kuwepo njia ya wazi kuhusu suluhisho la mataifa mawili kwa Israel na Wapalestina. Nchi za Kiarabu zinaharakisha kutafuta njia mbadala ya pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuijenga upya Gaza.
(AFP, AP, DPA, Reuters)