Hamas, Israel kubadilishana tena mateka na wafungwa Jumamosi
1 Februari 2025Kundi la Hamas linatarajiwa kukabidhi mateka watatu wa Kiisrael leo Jumamosi, katika awamu nyingine ya kubadilishana mateka na wafungwa wa Kipalestina, chini ya mapatano yanayonuwia kufungua njia ya kumaliza vita vya miezi 15 Gaza.
Waisrael hao ni Yarden Bibas, baba wa mateka wadogo zaidi, Kfir, aliekuwa na miezi tisa wakati alipotekwa Oktoba 7, 2023, na Ariel ambaye alikuwa na miaka minne. Hamas ilisema mnamo Novemba 2023, kuwa watoto hao wavulana na mama yao Shiri, aliechukuliwa pia mateka, waliuawa katika shambulio la Israel.
Soma pia: Ramadhani yaanza bila usitishwaji vita Gaza
Raia wa Marekani na Israel Keith Siegel na mwingine wa Ufaransa na Israel Ofer Kalderon pia waatakuwa sehemu ya mabadilishano hayo ambamo Wapalestina 182 wataachiliwa huru kutoka magereza ya Israel.
Jumamosi hii pia itashuhudia Wapalestina wa kwanza wanaosafiri kutoka Gaza kwenda Misri kupitia kivuko kilichofunguliwa tena cha Rafah, wakiwemo wapiganaji 50 na raia 50 waliojeruhiwa, pamoja na watu wengine 100 watakaoruhusiwa kuvuka kwa misingi ya kiutu.