Hamas: Hakuna mazungumzo na Israel hadi wafungwa waachiwe
25 Februari 2025Katika taarifa yake, Bassem Naim, afisa wa ngazi ya juu wa Hamas amesema kundi hilo la wanamgambo limefuata kikamilifu vifungu vyote vya makubaliano, na kwamba hatua ya ucheleweshaji wa Israel kunayaweka makubaliano hayo katika hatari ya kusambaratika, na hivyo kusababisha kuzuka kwa vita.
Kama sehemu ya makubaliano, Israel ilitakiwa kuwaachia wafungwa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Hamas kuwaachia mateka wa Israel walioshikiliwa katika shambulizi la Oktoba 7, mwaka 2023.
Makubaliano ya kwanza kumalizika Jumamosi
Awamu wa kwanza ya kusitisha mapigano inatarajiwa kumalizika Jumamosi, na huku mazungumzo ya awamu ya pili yakiwa yanapaswa kuanza wiki kadhaa zilizopita, lakini bado hayajaanza.
Mwanadiplomasia wa Marekani anarejea kwenye mazungumzo wiki hii katika ukanda huo, huku akiwa na matumaini ya kuongeza muda wa awamu ya kwanza ili kuvuta muda kwa majadiliano zaidi, lakini Naim amesema Hamas haiko tayari kuzungumza hadi wafungwa hao waachiliwe huru.
Hayo yanajiri wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Sharren Haskel, akisema kuwa nchi yake inaweza kuongeza muda wa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas yanayotarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki hii, ingawa mazungumzo ya awamu ya pili yamekwama.
Matumaini ya mateka kuachiwa huru
''Nina matumaini suluhu itapatikana ili kuwaachia mateka, kama tulivyokubaliana, mateka wengine wanne katika siku chache zijazo. Hamas imekuwa ikikaidi makubaliano waliyosaini, ikiwa ni pamoja na kuahidi kutowatesa mateka na kuwaonyesha hadharani kama wanavyofanya,'' alifafanua Haskel.
Haskel amewaambia waandishi habari Jumanne kuwa hakuna uhalisia kwa pande hizo mbili kufikia makubaliano ya duru ya pili katika siku zijazo. Amesema hilo ni jambo linalopaswa kujadiliwa kwa undani, na litachukua muda mrefu.
Wakati huo huo, Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa amesisitiza umuhimu wa utawala wa sheria, na kusema kwamba serikali inakusudia kuanzisha kamati ya muda itakayotoa haki pamoja na kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wote wanaotuhumiwa kutenda udhalimu dhidi ya watu wa Syria.
Akiwahutubia takribani watu 600 wakati akiufungua mkutano kuhusu Majadiliano ya Kitaifa unaofanyika mjini Damascus, Al-Sharaa amewataka Wasyria kuungana pamoja na kushirikiana ili kuijenga nchi yao baada ya miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Soma zaidi: Syria yaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa
Mkutano huo wa kujadili mustakabili wa Syria, umehudhuriwa na wawakilishi wa vyama vya kiraia, jumuia za kidini na mirengo tofauti ya kisiasa.
Ama kwa upande mwingine, mamia ya watu wamehudhuria mazishi ya Oded Lifshitz, aliyeuawa akiwa anashikiliwa mateka katika Ukanda wa Gaza. Lifshitz, mwanaharakati wa amani, aliyekuwa na umri wa miaka 84, ni miongoni mwa watu 250 waliotekwa wakati wa mashambulizi ya kusini mwa Israel, Oktoba 7, 2023.
(AFP, AP, DPA; Reuters)