Hamas iko tayari kwa makubaliano yatakayositisha vita Gaza
2 Julai 2025Hamas imesema inashikilia msimamo wake wa muda mrefu, kwamba makubaliano yoyote ni lazima yajumuishe kusitisha kikamilifu vita katika Ukanda wa Gaza.
Kundi hilo limependekeza kuwa tayari kukubali usitishaji mapigano na Israel, lakini bado halijakubali mpango ulioungwa mkono na Marekani uliotangazwa na Rais Donald Trump hivi karibuni, likisema linashikilia msimamo wake wa muda mrefu, kwamba makubaliano yoyote ni lazima yajumuishe kusitisha kikamilifu vita katika Ukanda wa Gaza.
Awali rais Trump, alisema Israel imekubali kusitisha vita kwa siku 60 mjini Gaza, na kulihimiza kundi la Hamas kuridhia mpango huo kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Israel, Hamas watofautiana usitishaji wa vita Gaza
Rais huyo wa Marekani amesema siku hizo 60 zitatumika kuendeleza juhudi za kumaliza kabisa vita, jambo ambalo Israel inasema haitowezekana hadi ilisambaratishe na kulishinda kundi la Hamas.
Rais Donald Trump amekuwa akitoa shinikizo kwa pande hizo mbili hasimu kufikia makubaliano ya usitishwaji mapigano, kuachiwa mateka wanaoshikiliwa na kundi hilo na kusitisha kabisa vita hivyo vilivyodumu kwa takriban miaka miwili.