Hali yaripotiwa kurejea ya kawaida mjini Uvira, DR Kongo
26 Agosti 2025Ukiwa unapatikana kwenye kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, mji wa Uvira ni mji wa pili kwa jimbo la Kivu Kusini na wenye umuhimu mkubwa wa kiuchumi si tu kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lakini pia kwa nchi nyingine zinazopakana na Ziwa Tanganyika. Uvira ni kama kitovu cha kijamii na kiuchumi, kitovu cha biashara na huduma, lakini pia kitovu cha kilimo na mifugo Kivu Kusini.
Hata hivyo, mji huo uko kwasasauko katika hatari ya vitisho kutoka kwa makundi yenye silaha, na hasa vita vya AFC/M23 wanaodaiwa kusaidiwa na Rwanda dhidi ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linalosaidiwa na kundi linalojiita Wazalendo na jeshi la Burundi.
Licha ya wasiwasi, hali ya utulivu imeshuhudiwa katika mji huo leo mchana kinyume na ilivyokuwa jana na hata pia leo usiku, ambapo milio ya risasi ilisikika katika baadhi ya kata za Uvira hadi mapema asubuhi.
John Karume ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kiusalama katika Jimbo la Kivu Kusini, anakumbusha kwamba mji wa Uvira unapelekea majimbo memngine ya Kongo lakini pia anahisi kwamba tishio dhidi ya mji wa Uvira pia ni tishio dhidi ya nchi jirani ya Burundi inayoshirikiana na jeshi la Kongo kupambana dhidi ya AFC/M23.
Mji wa Uvira pia ni wa kimkakati kwa sababu ya bandari yake ya Kalundu, ambayo ni ya pili kwa ukubwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ambayo inarahisisha usafiri wa bidhaa kati ya Kongo na nchi za mashariki na kusini mwa Afrika.