Hali ya utulivu yarejea kijiji cha Kavuma Kongo
14 Aprili 2025Mashirika ya kiraia ya eneo hilo yanazungumzia kuhusu vifo vya watu wasiopunguwa saba wakiwemo raia watano na watu waliojeruhiwa wanaotibiwa katika vituo vya afya vya Kavumu.
Wapiganaji hao wa Wazalendo walijaribu kuuteka uwanja wa ndege wa Kavumu kwa dakika chache kabla ya kutimuliwa kwa nguvu na vikosi vya M23.
Kwa mujibu wa vyanzo vya asasi za kiraia, Wazalendo walijaribu kuuteka uwanja wa ndege baada ya waasi wa M23 kuwahamisha askari wake ili kuongeza idadi yao kuelekea vijiji vya Katana, Kabamba katika wilaya ya Kabare hadi Kasheke na Lemera katika wilaya ya Kalehe.
Soma pia:Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF lalaani shambulio dhidi ya hospitali Goma
Mapigano mengine makali kati ya M23 na Wazalendo yalitokea jana Jumapili huko Burhale katika wilaya ya Walungu ambapo magari na nyumba zinazoshukiwa kuwahifadhi M23 zilichomwa moto na Wazalendo katika eneo linaloitwa Mashango.
Wiki iliyopita, shambulizi lingine la Wazalendo dhidi ya mji wa Goma lilisababisha watu wasiopunguwa 50 kupoteza maisha. Taarifa ya gavana wa Kivu Kaskazini chini ya utawala wa M23 ilisema kwamba Wazalendo hao walisaidiwa na Jeshi la jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kongo yapuuza tuhuma
Hata hivyo, msemaji wa Jeshi la Kongo, Jenerali Sylvain Ekenge ametupilia mbali tuhuma hizo za M23, akizitaja kuwa ni njama za kuendeleza mauaji dhidi ya raia.
"Taarifa kwa vyombo vya habari ya AFC/M23, ambayo ilitayarishwa tangu mwanzo, ni hali halisi iliyofanywa kwa makusudi, sio tu kuficha na kuhalalisha mauaji ya kila siku ya raia katika mji wa GOMA, bali pia kuchezea maoni ya umma na kukidhi tamaa zao za uhalifu. Hii ni mbinu iliyopangwa kujaribu kukwamisha mipango yote ya amani inayoendelea.”
Haya yakijiri, Umoja wa Afrika ulimteua rasmi juzi Jumamosi, Faure Essozimna Gnassingbé, Rais wa Jamhuri ya Togo, kuwa mpatanishi mpya katika mchakato wa amani wa kutatua mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma pia:Kongo yatahadharisha kuhusu Kimeta kwa wanyama
Uamuzi wa Baraza Kuu la AU, uliopitishwa Jumamosi kwa utaratibu wa ukimya, unaashiria hatua muhimu katika juhudi za kuleta utulivu katika eneo hilo.
Kulingana na AU, Tume ina jukumu la kutengeneza ramani ya pamoja kwa kushauriana na pande zinazohusika. Mbinu hii inalenga kufaidika na matokeo yaliyopatikana wakati wa michakato ya upatanishi huko Luanda na Nairobi. Lakini hadi wakati huo, jina hili la Faure Gnansinbé halina kauli moja miongoni mwa mashirika ya kiraia nchini Kongo.