EU: Hali ya Ukanda wa Gaza inazidi kuzorota
7 Agosti 2025Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya amezungumzia hali hiyo ya Gaza katika mahojiano na shirika la habari la Reuters baada ya idara zinazohusika sera ya kigeni na masuala ya kiutu kutoa ripoti zao kwa mataifa wanachama jana usiku kuhusiana na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na Israel mwezi uliopita kuhusiana na upatikanaji wa misaada ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza.
Afisa huyo ambaye hakutajwa jina alianza kwa kueleza kwamba zipo hatua zilizopigwa kuanzia kwenye upatikanaji wa mafuta, kufunguliwa kwa baadhi ya njia hadi ongezeko la idadi ya malori yanayoingia kila siku kwenye eneo hilo lililozingirwa na ukarabati wa baadhi miundombinu muhimu.
Lakini, kwa upande mwingine alisema kuwa zipo sababu kubwa zinazoendelea kuzuia na kudhoofisha shughuli za kibinadamu na misaada kupelekwa Gaza, na hasa kutokana na mazingira mabovu yanayozuia usambazaji wa misaada kwa kiwango kikubwa.
Huzuni na vilio vyazidi kuhanikiza Gaza
Ameyasema hayo, wakati vilio vikizidi kuhanikiza kote kwenye Ukanda wa Gaza kufuatia hali mbaya ya kiutu na hasa janga la njaa. Miongoni mwao ni Ibrahim al-Najjar aliyempoteza mwanae wa miaka mitano Naim kutokana na utapiamlo mkali unaosambaa Gaza. Mwaka mmoja baadae, bado anamlilia mwanae huyo, na maumivu yanazidi kumuelemea kwa kuwa pengine atampoteza mwanae mwingine kutokana na njaa.
"Nilifiwa na mtoto wa kiume wa miaka mitano, jina lake Naim Ibrahim al-Najjar, alifariki katika hospitali ya Kamal Adwan kwa utapiamlo na njaa. Naweza kukutumia picha zake, uone jinsi alivyokuwa na jinsi mifupa yake ilivyoonekana. Kwa wale wanaosema hakuna njaa hapa wanadanganya, waje waone."
Nchini Ujerumani, chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto cha Die Linke kimeitolea wito serikali ya shirikisho na majimbo kuwaleta nchini humo watoto wa Gaza na Ukingo wa Magharibi waliojeruhiwa vibaya na walioathiriwa na kiwewe ili wapate matibabu ya haraka.
Kiongozi wa chama hicho Ines Schwerdtner na mwanachama mwenza wa chama Charlotte Neuhäuser wamependekeza hatua hiyo kuchukuliwa chini ya mfumo wa uratibu uliotumika wakati wa kuwasambaza wagonjwa wa UVIKO-19 na kuwaokoa majeruhi kutoka Ukraine.
Watu 38 wauawa wakati wakitafuta misaada
Na huko Gaza kwenyewe, taarifa kutoka mjini Deir Al Balah, zimesema karibu watu 38 wameuawa usiku wa jana wakati wakitafuta misaada inayopelekwa na Umoja wa Mataifa na vituo vinavyoratibiwa na Israel kwa usaidizi wa Marekani. Jeshi la Israel limesema lililazimika kufyatua risasi za onyo wakati umati wa watu ulipokaribia vikosi vyake.
Watu wengine 25, wakiwemo wanawake na watoto kadhaa, waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel, hii ikiwa ni kulingana na duru za tiba za huko Gaza, ingawa Jeshi la Israel lilisema liliwalenga wanamgambo wa Hamas pekee.
Idadi ya vifo vya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza imeongezeka na kufikia 61,158, huku wengine 151,442 wakijeruhiwa, tangu mzozo kati ya Hamas na Israel ulipozuka Oktoba 7, 2023, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza jana Jumatano.