Hali itakuaje Leverkusen bila Wirtz na Alonso?
7 Mei 2025Leverkusen ambao walikuwa washindi wa kombe la shirikisho DFB Pokal na Ligi Kuu Bundesliga msimu uliopita bila kushindwa hata katika mechi moja, wataumaliza msimu huu katika nafasi ya pili baada ya Bayern Munich kuunyakua ubingwa zikiwa bado zimesalia mechi mbili na wakiwa wamewazidi kwa pointi 8.
Na sasa kulingana na vyombo vya habari Ujerumani na duru zilizo klabuni hapo, wakuu wa Leverkusen wanajiandaa kwa uwezekano wa kuondoka kwa wachezaji muhimu wa timu hiyo akiwemo Wirtz, beki Jonathan Tah, mshambuliaji Patrick Schick na kocha Alonso.
Mkataba hadi mwaka 2027
Wirtz mwenye umri wa miaka 22 anatazamiwa kutimkia Bayern Munich katika dirisha lijalo la msimu wa joto. Mjerumani huyo amelengwa kwa muda mrefu na Bayern.
Akiwa ana mkataba Leverkusen hadi mwaka 2027, huenda Wirtz akaipa timu yake pato la zaidi ya yuro milioni 100 iwapo atahama, huku gazeti moja la Ujerumani likiripoti Jumatano kwamba Wirtz angependelea kuhamia Bayern iwapo ataondoka Leverkusen.
Huku mustakabali wa Wirtz ukiwa haubainiki, uwezekano wa Xabi Alonso kuondoka ni mkubwa, ikizingatiwa kwamba Muhispania huyo mara kadhaa amekataa kudhamiria kusalia Ujerumani kwa msimu mwengine.
Alonso mwenyewe amesema kutakuwa na mazungumzo kati yake na wakuu wake baadae msimu huu. Anatarajiwa pakubwa kujiunga na Real Madrid mara atakapoondoka kocha wa sasa Carlo Ancelotti ambaye anahusishwa na timu ya taifa ya Brazil.
Beki Jonathan Tah pia anaelekea kuihama klabu hiyo huku kandarasi yake ikiwa inaelekea kukamilika. Mwaka 2024 alikaribia kujiunga na Bayern Munich ila uhamisho ulivunjika katika dakika ya mwisho.
Mfungaji wa pili bora Bundesliga
Vilabu kadhaa vimehusishwa na Schick ikiwemo Barcelona inayofunzwa na Mjerumani na aliyekuwa kocha wake wa zamani wa timu ya taifa Hansi Flick.
Mshambuliaji wa Jamhuri ya Czeck Patrick Schick naye anadaiwa kwamba atajiunga na Tah katika kuihama Leverkusen huku akiwa hivi majuzi amelengwa sana na Bayern Munich, kuwa kama mshambuliaji msaidizi wa Harry Kane ambaye ndiye mfungaji bora wa Bundesliga msimu huu.
Schick amefunga mabao 19 katika Bundesliga msimu huu, akiwa mabao 5 nyuma ya Kane.
Chanzo: Reuters