Gutteres apongeza makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda
28 Juni 2025Pia alisifu uongozi wa Marekani katika kusimamia mazungumzo hayo ya upatanisho.Kauli hii inajiri baada ya mataifa hayo mawili ya Afrika kusaini makubaliano hayo siku ya Ijumaa mjini Washington, yakilenga kumaliza miongo kadhaa ya mapigano katika eneo la mashariki mwa Kongo.
Guterres alihimiza pande zote kutekeleza kikamilifu ahadi walizotoa katika mkataba huo, huku akisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia utekelezaji wake kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika na washirika wa kikanda na kimataifa.
Wakati huohuo, Umoja wa Afrika kupitia Mwenyekiti wa Tume, Mahmoud Ali Youssouf, ambaye alishuhudia utiaji saini wa mkataba huo, umetaja makubaliano hayo kuwa ni "hatua muhimu” katika kuleta amani, utulivu na maridhiano katika eneo hilo lenye migogoro kwa muda mrefu.
Makubaliano kati ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda yanajumuisha kuheshimu mipaka ya kitaifa, kusitisha uhasama, kusalimisha silaha na kuingiza makundi ya waasi katika mfumo rasmi. Pia yanakusudia kuwezesha kurejea kwa wakimbizi na watu waliopoteza makazi, pamoja na kuruhusu misaada ya kibinadamu kufika maeneo ya mzozo.