Guterres awatolea wito viongozi kufufua mipango ya maendeleo
30 Juni 2025Wito wa Guterres unatolewa wakati kukishuhudiwa upungufu wa ufadhili unaohatarisha mapambano dhidi ya umaskini na mabadiliko ya hali ya hewa. Aidha Guterres amesema:
"Lakini huu sio mgogoro tu wa idadi. Ni mzozo wa watu. Wa familia zinazokumbwa na njaa. Mzozo wa watoto kutopata chanjo. Wa wasichana wanaolazimishwa kuacha shule. Tuko hapa Seville kubadili mwelekeo. Kupiga jeki maendeleo na kuharakisha uwekezaji kwa kiwango na kasi inayohitajika."
Makumi ya viongozi wa dunia na zaidi ya wawakilishi 4,000 ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara, mashirika ya kiraia na taasisi za fedha wanakusanyika katika mji wa Seville kwa ajili ya mkutano wa siku nne wa kutafuta msukumo mpya kwa sekta ya misaada iliyokumbwa na mgogoro huku wakisaka pia njia za kukabiliana na pengo linalozidi kuongezeka baina ya nchi tajiri na masikini.