Guterres: Shambulizi dhidi ya wapalestina lichunguzwe
3 Juni 2025Wapalestina zaidi ya 30 waliuawa karibu na kituo hicho. Hii ni baada ya kikosi cha waokozi kudai kwamba vifo hivyo vilisababishwa na mashambulizi yaliyofanywa na Israel.
Katibu Mkuu huyo amesema kwenye taarifa yake kwamba amesikitishwa na mauaji hayo ya Wapalestina wa Gaza waliokuwa wakihangaika kupata msaada huko Ukanda wa Gaza. Akasema haikubaliki hata kidogo, kwamba raia hao wanayaweka hatarini maisha yao wakiwa wanatafuta chakula.
Guterres, akatoa wito wa uchunguzi wa haraka na ulio huru dhidi ya matukio hayo, na kuwawajibisha wahusika.
Starmer asikitishwa na kudorora hali huko Gaza
Na huko Glasgow, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema mapema leo kwamba hali katika Ukanda wa Gaza inazidi kudorora siku baada ya siku na kwa maana hiyo kuna umuhimu wa kuhakikisha eneo hilo la Kipalestina linapata misaada ya kiutu haraka iwezekanavyo.
Starmer amesema hayo alipoulizwa na waandishi wa habari akiwa Scotland kuhusiana na ikiwa Uingereza itachukua hatua yoyote kuhusiana na shambulizi linalodaiwa kufanywa na Israel jana Jumapili dhidi wa wakazi wa Gaza na kuwaua zaidi ya watu 30 na wengine 170 kujeruhiwa.
"Hali katika Ukanda wa Gaza inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku. Niwe wazi kwa kusema ni jambo lisilovumilika na kuna haja ya kusitishwa mapigano. Niwe wazi pia kwamba misaada ya kibinadamu inatakiwa kuingia kwa kasi na kwa wingi. Na, bila shaka, kuendelea kuhakikisha mateka waliozuiliwa kwa muda mrefu sana wanaachiliwa. Tunafanya kazi pamoja na washirika katika hilo."
Shuhuda: Niliona kwa macho yangu watu wakifa
Shuhuda mmoja aliyekuwepo wakati shambulizi hilo lilipofanywa huko Rafah, Sameh Hamuda ameliambia shirika la habari la AFP kwamba akiwa njiani na kundi jingine kubwa kuelekea kwenye kituo hicho cha misaada, ghafla droni na vifaru vikaanza kuwafyatulia risasi. Akasema watu wengi walikufa palepale akitizama.
Jeshi la Israel, IDF hata hivyo limesema uchunguzi wa awali umegundua vikosi vyake havikuwafyatulia risasi raia walipokuwa wakilikaribia eneo hilo la misaada.
Na badala yake, msemaji wake Effie Defrin amesema kupitia ujumbe wa vidio kwamba Hamas inafanya kila linalowezekana kuwazuia kugawa misaada na kuapa kuchunguza kila madai yanayotolewa dhidi ya IDF.
Taarifa za mchana huu pia zimesema IDF imeshambulia jengo la makazi katika eneo la Deir Al-Balah huko Ukanda wa Gaza na kuwaua watu 14, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, hii ikiwa ni kulingana na maafisa wa afya. Hata hivyo jeshi hilo halikutaka kuzugumzia shambulizi hilo lilipoombwa kufanya hivyo.