Guterres: Mauaji ya Wapalestina 27 yachunguzwe
3 Juni 2025Jeshi la Israel limesema Jumanne (03.05.2025) kwamba linachunguza ripoti za majeruhi katika tukio la ufyetuaji wa risasi kuwalengwa Wapalestina waliokuwa wakielekea kwenda katika kituo cha utoaji msaada wa chakula. Mamlaka za Hamas zilithibitisha awali kwamba Wapalestina wasiopungua 24 walikuwa wameuliwa karibu na mji wa kusini wa Rafah na wengine kadhaa wakajeruhiwa Jumatatu, lakin idadi hiyo sasa imefikia 27.
Awali lilisema lilifyetua risasi kuwalenga washukiwa waliowakaribia wanajeshi wake mapema Jumapili na Jumatatu, wakati maafisa wa afya na watu walioshuhudia waliposema watu 34 waliuliwa. Jeshi la Israel linakanusha kuwafyetulia risasi raia wala kuwazuia kufika katika kituo hicho cha misaada.
Wakfu wa utoaji misaada Gaza, unaokiendesha kituo hicho, umesema hakujawahi kutokea machafuko ndani wala katika maeneo yanayokizunguka. Wakfu umekiri Jumanne kwamba jeshi la Israel linachunguza ikiwa raia walijeruhiwa baada ya kuvuka eneo maalumu la usalama lililotengwa na kuingia eneo la shughuli za kijeshi, eneo ambalo liko nje ya eneo lao salama la utoaji wa misaada.
Guterres ataka uchunguzi huru ufanyike
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito uchunguzi huru ufanyike kufuatia madai ya mashambulizi ya Israel karibu na vituo vya usambazaji chakula huko Gaza. Guterres amesema haikubaliki kwamba Wapalestina wanahatarisha maisha yao kwa ajili ya chakula, akiongeza kuwa Israel ina wajibu chini ya sheria ya kimataifa ya utoaji misaada ya kibinadamu kuratibu na kusimamia upelekaji na utoaji misaada.
Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa, alisema, "Haikubaliki kwamba Wapalestina wanahatarisha maisha yao kwa ajili ya chakula. Kuingia kwa msaada kwa kiwango kikubwa ili kukidhi mahitaji makubwa ya watu Gaza lazima kurejeshwe mara moja na Umoja wa Mataifa lazima uruhusiwe kufanya kazi kwa usalama chini ya masharti yanayoheshimu kikamilifu kanuni za kibinadamu."
"Katibu Mkuu anaendelea kutoa wito wa usitishaji mapigano mara moja, wa kudumu na endelevu. Mateka wote lazima waachiliwe mara moja na bila masharti. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha usalama kwa wote. Hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo huu." Aliongeza kusema Dujarric.
Antonio Guterres ataka uchunguzi huru wa mauaji ya Wapalestina Rafah
Jeshi la Israel limekanusha madai hayo likisema uchunguzi uliofanywa na jeshi haukupata ushahidi wowote wa mashambulizi dhidi ya raia karibu ama ndani ya vituo vya misaada. Madai hayo hayakuweza kuthibitishwa.
Kauli ya Guterres imeibua ukosoaji mkali kutoka kwa serikali ya Israel. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Israel Oren Marmorstein ameieleza kauli hiyo kuwa ni fadheha na kumkosoa mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kwa kukosa kulitaja kundi la wanamgambo wa kipalestina la Hamas au kukataa kwake usitishaji mapigano na mapendekezo ya kuachiliwa huru kwa mateka.
Wajerumani hawataki Israel iuziwe silaha
Wakati hayo yakiarifiwa, matokeo ya utafiti wa maoni yaliyochapisha hivi leo yanaonyesha kwamba idadi kubwa ya Wajerumani wanaunga mkono kusitisha uuzaji silaha kwa Israel kutokana na vita vinavyoednelea Gaza. Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 58 ya walioulizwa waliunga mkono usitishaji kwa muda upelekaji silaha kwa Israel, huku wengine asilimia 22 wakipinga. Wajerumani wengine asilimia 19 hawakutoa uamuzi wao ama walikataa kujibu.
Utafiti huo wa maoni uliofanywa na kampuni ya kukusanya maoni ya INSA, iliyopewa kazi hiyo na shirika la uanaharakati la Avaaz, uliwajumuisha watu 1,001 waliohojiwa kati ya Mei 28 na Mei 30. Uuzaji na upelekaji silaha za Ujerumani nchini Israel umeendelea kumulikwa katika wiki za hivi karibuni kutokana na mzozo wa kibinadamu unaoendelea kushuhudiwa Gaza.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Johann Wadephul alitangaza siku chache zilizopita mchakato wa kudurusu upya upelekaji silaha ili kubaini ikiwa unaaendana na kuheshimu sheria ya kimataifa.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Alexander Dobrindt, kwa upande wake ameunga mkono kuendelea na upelekaji wa silaha kwa Israel kama ilivyokubaliwa hapo awali.
Shirika la Avaaz linajieleza lenyewe kama mtandao wa kimataifa wa kampeni unaolenga kushawishi maamuzi ya kisiasa kupitia hamasa ya raia.