Guterres alikataa pendekezo la Trump kuhusu Gaza
6 Februari 2025Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelikataa pendekezo la rais wa Marekani Donald Trump la Marekani kulidhibiti eneo la Palestina la Gaza na kuwahamisha watu wake wote. Katika mkutano na waandishi habari siku ya Jumanne akiwa pamoja na waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Trump kwa mshangao mkubwa alipendekeza umiliki wa muda mrefu wa Gaza na Marekani na kuibua ukosoaji kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Akizungumza kwa kamati ya Umoja wa Mataifa inashughulikia haki za Wapalestina, Guterres amesema kimsingi utekelezaji wa haki za Wapalestina unahusu haki ya Wapalestina kuishi kama binadamu katika nchi yao huru, lakini tumeshuhudia haki hizo zikikabwa koo na kutupiliwa mbali. Guterres amesisitiza suluhisho la mataifa mawili huku Israel na Wapalestina wakiishi kwa amani.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alipoulizwa kuhusu pendekezo la Trump amesema hatua yoyote ya kuwahamisha watu Gaza ni safisha safisha ya kikabila. Amesisitiza juu ya umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa na kuepusha aina yoyote ya safisha safisha ya kikabila.
Kufuatia ukosoaji wa kimataifa maafisa wa utawala wa Trump walionekana wakirudi nyuma kuhusu pendekezo la Trump, wakisema hatua yoyote ya kuwaondoa Wapalestina kutoka Gaza itakuwa ya muda tu, wakati eneo kubwa lililoharibiwa likijengwa upya. Pia walisema Trump hakutoa hakikisho la kupeleka wanajeshi Gaza kutekekeleza mpango wake.
Ukosoaji wa kimataifa
Mjumbe wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour ameitisha mkutano wa kimataifa wenye tija katika Umoja wa Mataifa kujadili suala hilo, uliopangwa kufanyika mwezi Juni huku Saudi Arabia na Ufaransa zikiwa wenyekiti wenza. Mansour amesisitiza msimamo wa Wapalestina kuupinga na kuukataa mpango wa Trump wa kulitwaa eneo la Gaza na hawataondoka Gaza kwa kuwa ni sehemu ya nchi yao na hawana nchi nyingine mbali na dola la Palestina.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi wamesema hatua yoyote ya kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza au Ukingo wa Magharibi haitakubalika. Kwa mujibu wa taarifa ya afisi ya rais wa Ufaransa, viongozi hao wawili wameyasema hayo baada ya mazungumzo yao ya simu jana Jumatano wakisema itakuwa ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa, kikwazo kwa suluhu la mataifa mawili na nguvu kubwa ya kudhoofisha utulivu kwa Misri na Jordan.
Al-Sisi amemwambia Macron kwamba jumuiya ya kimataifa lazima ibebe dhamana isaidie utekelezaji wa mpango wa suluhisho la mataifa mawili katika kuutanzua mzozo baina ya Israel na Wapalestina.
Soma pia: Trump asema Marekani itachukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza
Canada imesema msimamo wake wa muda mrefu kuhusu Gaza haujabadilika. Waziri wa mambo ya nje wa Canada Melanie Joy amesema katika taarifa aliyoiandika siku ya Jumatano kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba Canada bado inaheshimu na imejitolea kwa dhati kwa juhudi za kupatikana suluhisho la mataifa mawili.
Maandamano ya kumpinga Trump Marekani
Maalfu ya waandamanaji walikusanyika katika miji mbalimbali ya Marekani hapo jana kupinga mipango ya awali ya utawala wa Trump, wakilalamika kuhusu hatua kali dhidi ya uhamiaji, ukandamizaji wa haki za watu waliozaliwa na jinsia tata na pendekezo la kuwahamisha Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.
Waandamanaji huko Philadelphia katika miji mikuu ya majimbo ya Minnesota, Michigan, Texas, Wisconsin, Indiana na kwingineko, walibeba mabango kumpinga Trump na bilionea Ellon Musk, kiongozi wa idara mpya ya Trump inayoshughulikia utendaji na mradi wa mwaka 2025 wa serikali ya Marekani na jamii ya Wamarekani.
(afp, reuters)