Guterres aitaka Israel kujizuia kuidhibiti Gaza
29 Agosti 2025Akizungumza Alhamisi na waandishi habari, Guterres amesema maelfu ya raia wa Gaza watalazimika kukimbia tena, na kuzitumbukiza familia katika hatari kubwa zaidi.
Amerudia wito wake wa kusitishwa mapigano mara moja, akisema tangazo la Israel kuhusu nia yake ya kuidhibiti Gaza, linaashiria hali mpya ya hatari.
Amesema njaa ya raia haipaswi kamwe kutumika kama silaha ya kivita na kutoa wito wa kuwepo upatikanaji wa misaada ya kiutu.
Siku ya Jumatano, msemaji wa jeshi la Israel alitangaza kwamba maandalizi yalikuwa yanaendelea kwa ajili ya mpango wa kuwahamisha wakaazi wa Gaza.
Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich ameitaka serikali ya nchi hiyo kuanza kujinyakulia sehemu ya maeneo ya Ukanda wa Gaza, iwapo kundi la wanamgambo la Kipalestina la Hamas, litaendelea kukataa kuweka chini silaha.