Guterres aisihi Israel kusitisha ujenzi Ukingo wa Magharibi
21 Agosti 2025Guterres ameeleza kwamba mpango huo unakiuka sheria za kimataifa na unapingana na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Guterres, Stephane Dujarric, kupitia taarifa amesema mwendelezo wa mradi huo wa ujenzi wa makaazi ni kitisho cha kimsingi kwa suluhisho la mataifa mawili.
Mapema jana, kamati ya mipango ya Israel iliidhinisha mpango wa kujenga takriban nyumba 3,400 katika eneo la E1, kipande muhimu cha ardhi kilichopo kati ya Jerusalem Mashariki na makaazi ya Maale Adumim.
"Uamuzi wa mamlaka ya Israel wa kupanua ujenzi wa makaazi haramu, ambao utagawanya Ukingo wa Magharibi, lazima ubatilishwe. Ujenzi wote wa makaazi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa."
Mradi huo wa ujenzi wa makaazi utaugawanya Ukingo wa Magharibi mara mbili; upande wa kaskazini na kusini, na kuufanya mpango wa kuanzishwa taifa huru la Palestina kuwa mgumu.
Mpango huo wa Israel pia umekosolewa vikali na mataifa kama Ufaransa, Canada na Australia, ambayo yanapanga kulitambua rasmi taifa la Palestina mnamo mwezi Septemba.