Guterres ahofia kuongezeka kwa mzozo wa DRC
24 Januari 2025Katika taarifa yake, msemaji wa Guterres, Stephane Dujarric, amesema kuwa katibu huyo mkuu amesikitishwa na kuanza tena kwa mapigano na kulaani vikali mashambulizi hayo mapya yaliyoanzishwa na kundi hilo la M23 tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Kauli hii inajiri wakati hali ya mambo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inazidi kuwa mbaya, ambapo milio ya risasi na miripuko inaendelea kusikika karibu na mji muhimu wa Sake ulio umbali wa kilomita 20 kutoka mji mkuu wa Goma.
DRC: Maelfu ya watu wakimbia baada ya M23 kuingia Sake
Shughuli mbalimbali, zikiwemo shule, zimekatizwa kote katika mji wa Goma asubuhi ya leo, ingawa Jeshi la Kongo linasema bado linapigana kuwazuia waasi wa M23 kusonga mbele kuelekea Goma.
Waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wanapambana na jeshi la Kongo na wameimarisha udhibiti wao katika maeneo yanayoizunguka Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Kongo, katika ghasia ambazo zimewalazimu takriban watu 230,000 kuyakimbia makaazi yao.
Rwanda imeendelea kukanusha taarifa za kuliunga mkono kundi la M23.