Guterres ahimiza juhudi kutimiza suluhisho la mataifa mawili
30 Aprili 2025Guterres ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ahadi hiyo ya suluhisho la mataifa mawili iko hatarini kutoweka kabisa.
Ameongeza kuwa utashi wa kisiasa wa kufanikisha lengo hilo unaonekana kuwa mbali zaidi sasa kuliko wakati wowote ule.
Soma pia: Mkuu wa UN Guterres asema Gaza imegeuka uwanja ya mauaji
"Muda unakwenda. Suluhisho la mataifa mawili liko karibu kufikia hatua isiyoweza kurudi nyuma. Jamii ya kimataifa ina jukumu la kuzuia ukaliaji wa kudumu na vurugu."
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehimiza mataifa kuchukua hatua zaidi, kando na kutoa kauli tu na kueleza hatua mahsusi za kufufua suluhisho la mataifa mawili.
Amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika ukanda wa Gaza ambapo karibu Wapalestina 2,000 wameuawa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Machi yaliposambaratika.