Guterres aahidi msaada wa kuijenga upya Ukraine
1 Julai 2025Wizara ya ulinzi ya Urusiimesema vikosi vya ulinzi wa anga vimeziharibu droni 60 za Ukraine usiku wa kuamkia leo. Nyingi ya droni hizo ziliharibiwa katika anga ya maeneo ya kusini magharibi mwa Urusi na Rasi ya Crimea, Bahari Nyeusi na Bahari ya Azoz.
Haya yamejiri baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuahidi msaada kwa Ukraine katika juhudi za kuijenga mpya nchi hiyo iliyovamiwa na Urusi miaka mitatu iliyopita.
Katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal, katika mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa kuhusu ufadhili wa fedha kwa ajili ya maendeleo mjini Seville kusini mwa Uhispania, Guterres alisisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa kuiunga mkono kwa dhati serikali ya Ukraine kushughulikia mahitaji ya kibinadamu, ujenzi na kuufufua uchumi.
Guterres pia alisisitiza umuhimu wa kupata usitishaji mapigano mara moja na usio na masharti nchini Ukraine.