GULFPORT,MISSOURI:Kimbunga Katrina kimeshaua watu 55 hadi sasa.
30 Agosti 2005Kiasi cha watu 55 wanahofiwa wamekufa baada ya kimbunga kilichopewa jina Katrina kuyakumba maeneo ya kusini mwa Marekani.Kimbunga hicho ambacho inasemekana ni moja kati ya vimbunga vyenye nguvu kubwa kuwahi kupiga Marekani,kwa sasa kimepungua kasi yake na kuwekwa katika hadhi ya dhoruba ya tropiki.
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kutokea kwa vifo hivyo na watu wengi wamenasa katika vifusi vya nyumba zilizobomolewa na kimbunga hicho.
Katika majimbo ya Mississippi,kimbunga cha Katrina kimesababisha viwanja vya ndege kufungwa na pia umeme umakatika katika maelfu ya nyumba.
Maafa makubwa pia yameripotiwa katika majimbo ya jirani ya Alabama na Louisiana,ambapo kimbunga hicho kilipiga kikitokea Ghuba ya Mexico.
Mji wa New Orleans haukupata madhara makubwa ya kimbunga hicho kama ilivyodhaniwa kabla,lakini kumetokea mafuriko makubwa.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imepeleka waokoaji kutoka kikosi chake cha wanamaji,kusaidia kazi ya kuwatafuta na kuwaokoa watu ambao hadi sasa hawajulikani walipo.