Guinea:Aliyekuwa kiongozi wa kijeshi asemehewa kwa mauaji
29 Machi 2025Kiongozi wa kijeshi wa Guinea Conakry, Mamady Doumbouya amemsamehe kiongozi wa zamani wa kijeshi wa nchi hiyo, Moussa Dadis Camara kwa sababu za kiafya, Mwaka uliopita mahakama ilimkuta Camara na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa mauaji ya mwaka 2009. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa televisheni ya taifa nchini humo.
Camara, ambaye alichukua mamlaka kwa njia ya mapinduzi 2008, alihukumiwa Julai 31, 2024 kifungo cha miaka 20 jela kwa kuhusika katika mauaji ya watu wasiopungua 157 wakati wa maandamano ya kuunga mkono demokrasia katika uwanja wa michezo mjini Conakry.
Soma zaidi: Tetemeko: Juhudi za uokoaji zaendelea Myanmar na Thailand
Mnamo mwaka 2009, maelfu ya watu waliokuwa wamekusanyika kumshinikiza Camara asigombee katika uchaguzi wa rais walipigwa risasi, kuchomwa visu na kupigwa huku vikosi vya usalama vikifyatua mabomu ya machozi na kuwafungulia mashtaka.
Siku ya Alhamisi serikali ya kijeshi ya taifa hilo la Afrika Magharibi ilitangaza kulipa fidia kwa waathirika wa mkasa huo kama ilivyoamuliwa na mahakama.