Grossi aonya kuwepo kwa dunia yenye mataifa 25 ya nyuklia
7 Septemba 2025Akizungumza na gazeti la Italia La Repubblica, Grossi alisema hatari ya mzozo wa nyuklia leo ni kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa zamani, huku mchakato wa kupunguza au kuondoa silaha hizo ukiwa umekwama.
Kwa sasa kuna mataifa tisa yenye silaha za nyuklia ambayo ni Marekani, Urusi, Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, Korea Kaskazini na Israel, lakini Grossi ameonya kwamba baadhi ya viongozi wa nchi muhimu Asia na Ghuba ya Uajemi wameonyesha nia ya kujiunga na orodha hiyo.
Amesema mataifa yenye silaha hizo yanazalisha zaidi, ikiwemo China, hali aliyoitaja kuwa ya kutisha. Kulingana na ripoti kutoka taasisi ya utafiti wa amani ya SIPRI na taarifa kutoka Kampeni ya Kimataifa ya Kuondoa silaha za Nyuklia, ICAN, kwa sasa kuna makadirio ya silaha 12,000 za nyuklia duniani, ambapo Marekani na Urusi pekee zinamiliki zaidi ya 10,000.