GHF: Tunasitisha huduma kwa muda Gaza
4 Juni 2025Shirika la misaada ya kibinadamu linaloungwa mkono na Marekani la GHF limesema kwamba halitosambaza misaada yoyote kwa watu wa Gaza siku ya Jumatano (04.06.2025) ili kujadiliana na jeshi la Israel namna ya kuongeza hatua zaidi za kiusalama katika vituo vya kutolea misaada, hayo yamesemwa na msemaji wa shirika hilo.
Hatua hiyo inajiri baada ya jeshi la Israel kusema ilifanya mashambulizi karibu na vituo vya kutolea misaada vya shirika hilo siku ya Jumanne (03.06.2025)ambapo shirika la Msalaba Mwekundu limesema watu 27 waliuawa na wengine zaidi ya 150 kujeruhiwa.
Wakfu huo unaoungwa mkono na Marekani unapingwa na Umoja wa Mataifa na mashirika kadhaa ya misaada ya kiutu.
Umoja wa Mataifa umelaani matukio hayo na kusema yanaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.